Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu
Tarehe 10 Disemba imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu, siku ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) lilipasisha tangazo la Kimataifa la Haki za Binadamu mwaka 1948. Kwa mnasaba huo tumewaandalia kipindi maalumu chini ya anwani: "Haki zisizo za binadamu, kwa mnasaba wa siku hiyo.
Katika kipindi chetu hiki, tutajadili na kuwabainishia historia kuhusu haki za binadamu, kisha tutazungumzia sababu za kuitangaza tarehe 10 Desemba kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu. Pia tutaangalia ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni.
Haki za binadamu ni haki za msingi zaidi na za asili ambazo kila binadamu anapaswa kuwa nazo kiasili na kwa sababu tu ya kuwa binadamu. Ni haki ambazo wanadamu wanapaswa kuwa nazo bila kujali rangi, jinsia na imani zao, wakati wote na mahali popote. Haki hizi zimeathiriwa na silsila ya kanuni ambazo katika zama za sasa zimekuwa matamko, sheria na maazimio ambayo yana sura ya kimataifa na yanawakilisha misingi ya kiroho ya ustaarabu wa kisasa wa binadamu. Kanuni hizi, ambazo baadhi yake zilijumuishwa mwanzoni katika Azimio la Haki za Kibinadamu lililoidhinishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1948, kwa hakika zimepata ilhamu kutokana na mafundisho ya dini kuu zinazompwekesha Mwenyezi Mungu katika karne nyingi zilizopita; na zilipaswa kumtambua mwanaadamu kuwa ni kiumbe mwenye hadhi, heshima na utukufu bila kujali rangi, utaifa, jinsia, imani, hali ya maisha ya kijamii na muundo wa mwili wake, kwa hivyo hazipasi kutumiwa kwa ajili ya kuwanyanyaswa wanadamu wengine kwa namna yoyote ile.

Kwa sababu hiyo, mashirika ya kimataifa yamepewa jukumu la kutekeleza na kusimamia utekelezaji wa sheria kuu ambazo zimeainishwa kwa ajili ya kudhamini uhai, uhuru na utu wa binadamu. Hata hivyo hadi sasa hakuna dhamana ya utekelezaji sahihi au kamili wa sheria hizo; na katika baadhi ya matukio utekelezaji wake umekuwa wa undumakuwili. Haki hizi, kwa sura yake pana, ni pamoja na afya, uhuru, maendeleo ya kibinafsi, haki ya kuchagua makazi na sera za maisha, utamaduni, kazi, haki ya kusaidiwa katika kijamii na usalama wa kudumu katika nyanja zote.
Mkutano wa kwanza wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa ulifanyika London Februari 16, 1946. Baraza hilo lilitoa azimio na kuasisi Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa azimio hilo, kamisheni hiyo ilitakiwa kuwasilisha kwa Katibu wa Baraza la Uchumi na Kijamii la Umoja wa Mataifa mapendekezo na ripoti kuhusiana na makubaliano ya kimataifa kuhusu uhuru wa raia, kuunga mkono jamii za waliowachache na kupiga marufuku ubaguzi wa jinsia, rangi, lugha na dini.
Mkutano wa Baraza la Kiuchumi na Kijamii ulifanyika ukiwa na timu ya uongozi wa kitaalamu katika haki za kiraia na kimataifa kwa lengo la kuandaa tamko la kimataifa kuhusu haki za bindamu, na hatimaye Azimio la Haki za Binadamu liliratibiwa baada ya miaka miwili, yaani mwaka 1948.
Baada ya kuandaliwa azimio hilo la haki za binadamu katika mkutano wa tarehe 10 Disemba 1949, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko Paris lilipasisha azimio hilo kwa kura 48 za ndio, wanachama 8 hawakupiga kura na hakukuwa na kura yoyote ya hapana. Hivyo tarehe 10 Disemba ikapewa jina la Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu linajumuisha utangulizi na vifungu 30. Katika kifungu cha kwanza kumeashiria usawa wa binadamu na moyo wa undugu kati ya binadamu wote.
Sehemu moja ya kifungu hicho inasema: "Binadamu wote wamezaliwa wakiwa huru na wako sawa katika suala la hadhi, utukufu na haki. Wote wana akili na dhamiri na wanapaswa kuamiliana kwa moyo wa udugu."
Licha ya kupasishwa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu, lakini hali halisi ilionekana kuwa tofauti katika upande wa utendaji, kwa sababu matukio mbalimbali yametukia tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia hadi leo, ambayo yanaonyesha kuwepo mwanya mkubwa kati ya malengo yaliyokusudiwa na utendaji wa jamii ya kimataifa katika suala la kutetea haki za binadamu. Kwa kadiri kwamba, kinyume na ilivyodhaniwa awali, nara na shaari za kutetea haki za binadamu zimegeuzwa na zinatumiwa na serikali za nchi za Magharibi kama wenzo wa kuzishinikiza kisiasa na kiuchumi nchi nyingine ili kufanikisha maslahi yao ya kikoloni.
Wapendwa wasikilizaji, mfano wa wazi wa ukiukwaji wa Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu unaonekana zaidi katika mienendo ya Marekani na utawala haramu wa Israel. Ingawa Marekani imekuwa ikijaribu kujiarifisha kama nchi inayounga mkono na inayoongoza katika uwanja wa haki za binadamu katika mashirika na taasisi za kimataifa, lakini kimsingi, nchi hiyo ni miongoni mwa nchi zilizo na mifumo dhaifu ya haki za binadamu duniani. Kuwatia watu nguvuni kiholela, kuziuzia silaha nchi zinazovunja haki za binadamu, umaskini na kukosekana usawa, ukatili wa kijinsia unaosababishwa na ubaguzi mkubwa wa rangi ulioenea nchini Marekani ni mifano michache tu ya jinai dhidi ya binadamu zinazofanywa na Marekani.
Utawala wa Kizayuni wa Israel sawa kabisa na Marekani, umetenda na unaendelea kutenda jinai za kutisha dhidi ya binadamu ambazo zote zinafanyika kwa uungaji mkono wa pande zote wa Marekani na washirika wake wa Kimagharibi.

Hivi karibuni Kamisheni ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikusanya ripoti kuhusu jinai muhimu zaidi zilizofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kipindi cha miaka 75 iliyopita. Sehemu ya kwanza ya ripoti hiyo inahusu orodha ya jinai za miaka 75 za utawala unaouwa watoto na wa kibaguzi (Apartheid) wa Israel, na sehemu ya pili inahusu maazimio ya Umoja wa Mataifa na Baraza la Haki za Binadamu dhidi ya utawala huo. Miongoni mwa jinai za hivi karibuni za Israel dhidi ya binadamu, ni mauaji yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Kwa mujibu wa ripoti ya hivi karibuni ya Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuuawa shahidi na kujeruhiwa zaidi ya watu elfu 45 katika siku 40 za awali za mashambulizi ya Isarel Ukanda wa Gaza, kuharibiwa majengo na miundombinu ya makazi ya maelfu ya raia, kulazimishwa watu zaidi ya milioni moja kuhama makazi yao, ni sehemu tu ya jinai ambazo utawala wa Kizayuni wa Israel umezitenda dhidi ya watu wasio na ulinzi wala hatia wa Gaza kwa kushirikiana na nchi inayojinadi kuwa mtetezi mkuu wa haki za binadamu duniani yaani, Marekani.
Ni vyema kufahamu kuwa katika kipindi cha miaka 75 tangu kuasisiwa utawala bandia wa Israel hadi mwaka 2022, maazimio 512 dhidi ya Israel yameidhinishwa na Baraza Kuu, Baraza la Usalama la UN na Baraza la Haki za Binadamu, ambapo Marekani imeyapigia kura ya veto maazimio 55 yaliyotolewa dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni.
Wapendwa wasikilizaji, tunatumai kuwa mmenufaika na yote tuliyoweza kuwaandalia juma hili katika kipindi hiki kilichowajia kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.