Umoja na Udugu wa Kidini katika Qur'ani na Hadithi
Suala la umoja katika umma wa Kiislamu, ni jambo lenye umuhimu mkubwa na ambalo limesisitizwa sana katika Qur'ani na Hadithi. Kinsingi ni kuwa umoja ni nguzo muhimu katika mafundisho ya Qur'ani na pia unachukuliwa kuwa moja ya misingi muhimu katika Hadithi za Mtume Muhammad (saw) na Ahlu Beit wake (as).
Siku hizi ni siku za maadhimisho ya kuzaliwa Mtume huyo mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw) na pia Wiki ya Umoja wa Kiislamu. Tunakupeni wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, mkono wa pongezi na fanaka kwa minasaba hii miwili muhimu. Kwa msingi huo, tumenuia kuzungumzia katika kipindi cha juma hili suala la umoja na udugu wa kidini katika Qurlani Tukufu huku tukimwomba Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe miongoni mwa wale wanaofanyia kazi mafundisho ya Qur'ani na Hadithi za Mtume wake (saw) ili tuweze kufanikisha na kuimarisha umoja na udugu katika umma wa Kiislamu. Bila shaka mtoaji wito wa kwanza wa kuwepo umoja na udugu katika Umma wa Kiislamu ni Qur'ani Tukufu. Moja ya masuala ambayo yamezungumziwa kwa kina na kusisitizwa katika kitabu hiki cha mbinguni ni suala la umoja wa Waislamu na kujiepusha kuzua hitilafu na mifarakano katika umma wa Kiislamu. Qur'ani inaashiria katika zaidi ya Aya 50 suala la kuwepo umoja na kujitenga na hitilafu pamoja na kubainisha njia za kuepuka hitilafu hizo na vilevile kuimarisha umoja kati ya Waislamu, suala ambalo bila shaka linadhiihirisha wazi namna kitabu hicho kitakatifu kinavyotilia mkazo jambo hilo. Wito huo wa kuwepo umoja miongoni mwa Waislamu sio nasaha wala pendekezo tu bali ni taklifu na wajibu. Kwa maana kuwa kama ambavyo Waislamu wana jukumu la kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja tu kwa msingi wa mafundisho ya Tauhidi pia wana jukumu la kufanya juhudi za kuleta umoja katika jamii ya Kiislamu.
Qur'ani Tukufu inauchukulia umoja kuwa neema kubwa na maalumu na kumchukulia Mwenyezi Mungu kuwa sehemu muhimu na ya msingi katika kupatikana umoja huo. Inawataka Waislamu na waumini kutafakari na kukumbuka historia chungu ya mgawanyiko na ghasia na kufanya juhudi za kulinda umoja wao, kwa sababu kuwepo umoja kati ya umma na waumini ni takwa muhimu la Mwenyezi Mungu. Qur'ani Tukufu inazitaja zama za ujahilia kuwa zama za mifarakano na hitilafu, zama ambazo baadaye zilibadilika na kuwa zama za umoja na kuhurumiana kutokana na neema ya Uislamu. Aya ya 103 ya Surat Aal Imran inasema: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui nyinyi kwa nyinyi, naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.
Kwa mtazamo wa Uislamu, ulimwengu umejengeka kwa msingi wa Tauhidi na umoja. Kutokana na kuwa Tauhidi ni jambo la kimaumbile, Waislamu wote wanalienzi jambo hilo na kwa hakika ndio msingi muhimu zaidi unaoziunganisha madhehebu zote za Kiislamu, bali dini zote za Mwenyezi Mingu. Kumwamini Mwenyezi Mungu mmoja huunganisha nyoyo za waumini na kuwafanya kuhurumiana na kushirikiana, ni kana kwamba wote wana moyo mmoja. Aya ya 92 ya Surat al-Anbiyaa inasema: Kwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu kwa hivyo niabuduni Mimi.
Kwa mujibu wa wafasiri wa Qur'ani Tukufu, maana ya umma mmoja ni umma ambao hauitilafiani na wote kuwa na neno moja kwa msingi wa Tauhidi. Hata hivyo tunapasa kuashiria hapa nukta hii muhimu kwamba hata kama umoja ni jambo la kimaumbile lakini linahitajia malezi na uzingatiaji maalumu, la sivyo, haliwezi kustawi kama inavyotakikana na huenda likakabiliwa na hatari ya kupotoshwa.
Udugu wa kidini au Kiislamu ambao unatajwa mara kwa mara katika Qur'ani una athari kubwa katika kuimarisha na kuleta umoja na mshikamano katika umma wa Kiislamu. Udugu huo wa kidini na Kiislamu umetajwa katika Aya nyingi za Qur'ani kuwa nguzo muhimu inayoeneza umoja wa Waislamu na kupambana na kila aina ya mifarakano na unafiki. Baada ya kuashiria kanuni hiyo kuu katika Surat Hujuraat, Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 9 ya Sura hiyo: Na ikiwa makundi mawili katika Waumini yanapigana, basi yapatanisheni. Anasisitiza zaidi suala hili katika Aya inayofuata na kutoa sababu za kuharakishwa jambo hilo kwa kusema: Hakika Waumini ni ndugu, basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu ili mrehemewe.
Aya hii inasisitiza kwamba waumini ni ndugu na hivyo wanapasa kuimarisha mapenzi kati yao na kwamba iwapo watatengana basi juhudi zifanyike kwa ajili ya kuwaleta pamoja. Inasema iwapo pande mbili au kadhaa za waumini hao zitagombana na kuhitilafiana basi hatua za haraka zichukuliwe na kundi moja miongoni mwao kwa ajili ya kufanya suluhu na kuzipatanisha pande hizo. Kama tulivyotangulia kusema, neema ya udugu wa Kiislamu ni neema kubwa zaidi ambayo Mwenyezi Mingu aliwatunuku waumini. Mwenyezi Mungu anazungumzia tena neema hiyo katika Aya ya 63 ya Surat Anfaal kwa kusema: Na akaziunganisha nyoyo zao. Na lau wewe ungelitoa yote yaliyomo duniani usingeliweza kuziunganisha nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaunganisha. Hakika Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu na Mwenye hikima.
Katia jamii ambayo ina makundi tofauti ya kimadhehebu, mirengo ya kisiasa, kiutamaduni na kadhalika, kuwepo hitilafu miongoni mwa wafuasi wa makundi na mirengo hiyo ni jambo la kawaida kabisa na pia kuwepo mijadala ya kielimu katika nyanja hizo ni jambo la kawaida. Kwa kawaida hitilafu hizo hutokea katika matawi na sio katika misingi ya imani na itikadi zinazohusiana na masuala hayo, na kwa hivyo hazipasi kuleta mgawanyiko wala kuzuia kupatikana umoja kati ya Waislamu. Na hasa inapotokea kwamba adui wa Uislamu anapanga njama za kudhoofisha na kuiangamiza jamii ya Kiislamu, Waislamu wote wanapasa kuweka kando tofauti zote za kibinafsi na maslahi ya kimakundi na kufanya jitihada za kuondoa hatari ya pamoja inayowakabili. Hii ni kwa sababu hitilafu za kimadhehebu na vita vya kikabila huhatarisha usalama wa umma wa Kiislamu na kuzuia kufikiwa malengo yake matukufu. Imam Ali (as) anawatahadharisha Waislamu kutohitilafiana na kutengana katika hotuba ya 176 ya Nahjul Balagha kwa sababu jambo hilo lina madhara makubwa kwa umma wa Kiislamu. Imam Ali mwenyewe hata kama alikuwa na haki ya wazi ya kuchukua uongozi wa umma wa Waislamu mara tu baada ya kuaga dunia Mtume Mtukufu (saw) kutokana na amri iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini alifumbia macho jambo hilo na kutopambana na makhalifa watatu waliotawala kabla yake ili kulinda umoja wa Waislamu. Aliamua kukaa kimya kuhusiana na jambo hilo kwa muda wa miaka 25 laikini pamoja na hayo alikuwa akishirikiana na makhalifa hao alipohitajika kufanya hivyo kwa lengo la kulinda umoja na maslahi makuu ya umma wa Kiislamu. Hii ni kwa sababu baada ya kuaga dunia Mtume (saw) kulidhihiri manabii wa uongo katika umma wa Kiislamu ambao walisababisha migogoro mikubwa katika jamii na hata kuwafanya baadhi ya watu waliokuwa wamesilimu karibuni kuritadi na kurudi katika imani zao potovu za zamani.
Nukta nyingine ya kuimarisha umoja wa Kiislamu ni kuchukua tahadhari na kujiepusha na taasubi pamoja na fikra mgando. Kwa maana kwamba kabla ya kufanya jambo lolote lile na kujishughuilisha na masuala ya kitaasubi, Waislamu wanapasa kutafakari juu ya athari zake hasi kwa umma wa Kiislamu. Hii ni kwa sababu taasubi ndio huwa mwanzo wa kutokea hitilafu na migawanyiko katika jamii ya Kiislamu. Kwa ibara nyingine, taasubi ni kushikilia misimamo ya kijahili na kutozingatia hoja za kimantiki, jambo ambalo husambaratisha misingi ya watu binafsi na pia ya jamii nzima, iwe ni taasubi za kimadhehebu, kikabila, kisiasa, kiutamduni au kivyama.