Nov 09, 2019 07:16 UTC
  • Wiki ya Umoja wa Kiislamu-1 (Mtindo wa Maisha ya Mtume SAW Katika Familia)

Assalaamu Alaykum wapenzi wasikilizajii popote pale mlipo. Tumo katika siku tukufu za sherehe za kuadhimisha maulidi na kuzaliwa Mtume Muhammad (saw).

 

Waislamu wa Kisuni wanategemea baadhi ya riwaya katika kuamini kwamba Mtume Mtukufu (saw) alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal huku Waislamu wa madhehebu ya Shia wana riwaya nyingine nyingi zinazowafanya waamini kuwa mtukufu huyo alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal. Kipindi cha kati ya tarehe hizo mbili kilitangazwa na Imam Khomeini (MA) kuwa Wiki ya Umoja wa Kiislamu ili kuleta umoja na mfungamano kati ya Waislamu bila kujali madhehebu zao. Kipindi hiki maalumu kinachojukieni kwa mnasaba wa kuanza wiki ya umoja ambapo kitazungumzia Mtindo wa Maisha wa Bwana Mtume SAW Katika Familia. Tafadhalini kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Moja ya zilizokuwa sifa muhimu za Mitume wa Mwenyezi Mungu ni utunzaji amana; hii ni kutokana na kuwa, Wajumbe hao wa Allah walikuwa na jukumu la kuwafikishia watu dini ya Mwenyezi Mungu na kuchunga siri za Mola Muumba. Utunzaji amana wa Bwana Mtume SAW ulianza kudhihiri tangu akiwa katika rika la ubarobaro na ujana wake. Watu wote walikuwa wakilitambua hilo na daima walikuwa wakimzungumzia. Sifa hii ndiyo iliyokuwa chimbuko la Mtume kuziteka nyoyo za watu na kuwafanya wasilimu na kuingia katika dini tukufu ya Kiislamu.

Ukweli, uaminifu na utunzaji wa amana wa Bwana Mtume SAW unatufanya sisi tusiwe na shaka na kigugumizi chochote katika kumfanya mbora huyu wa viumbe kuwa ni ruwaza njema na kiigizo cha maisha yetu. Hapana shaka kuwa, kufanya utafiti na uchunguzi kuhusiana na namna walivyoishi mawalii wa Mwenyezi Mungu, muamala na maingiliano yao na watu wengine ni jambo ambalo linatufanya sisi tujiunganishe na chanzo adhimu cha maarifa ya Mwenyezi Mungu na hilo kutufanya tustafidi na kunufaika na saada ya dunia na akhera.

Kwa kuzingatia kwamba, mwanadamu ameumbwa na Mwenyezi Mungu, hapana shaka kuwa, Muumba huyo amemuandalia mwanadamu huyu ratiba bora kabisa kwa ajili ya kuelekea katika ukamilifu. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 21 ya Surat al-Ah’zab:

لَقَدْ کَانَ لَکُمْ فِی رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن کَانَ یَرْجُو اللَّهَ وَالْیَوْمَ الآخِرَ وَذَکَرَ اللَّهَ کَثِیرًا

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.

 

Mtindo wa maisha wa Bwana Mtume SAW katika maneno na vitendo umekamilika na kujumuisha kila kitu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu anawataka wanadamu wamfanye Mtume SAW kuwa ruwaza na kiigizo chao katika maisha na watu wote wanaweza kuunda na kuratibu mtindo wao wa maisha kwa mujibu wa maneno, sira na mwenendo wa Bwana Mtume SAW. Kwa hakika tabia njema na maadili bora ya Bwana Mtume SAW ni ya kupigiwa mfano ambapo Mwenyezi Mungu analitambulisha hilo kama njia na kigezo cha mwanadamu.

Wapenzi wasikilizaji Bwana Mtume SAW alikuwa akiugawa wakati na muda wake katika makundi matatu: Muda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu yaani kwa ajili ya ibada, Swala na tahajudi. Sehemu nyingine ya muda wake kwa ajili ya familia yake ambapo alikuwa akikaa nao na kuzungumza nao sambamba na kuwadhaminia mahitaji yao ya lazima yakiwemo ya kiroho na kihuba. Na Sehemu ya tatu ya muda wake alikuwa akiutenga kwa ajili ya yake na watu na kuutumia kwa ajili ya kuwatatulia shida na hawaiji zao.

Kwa hakika jengo la familia msingi wake imara ni huba na mapenzi ndani ya familia hiyo. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 21 ya Surat ar-Rum:

وَمِنْ آیَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَکُم مِّنْ أَنفُسِکُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْکُنُوا إِلَیْهَا وَجَعَلَ بَیْنَکُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً إِنَّ فِی ذَلِکَ لَآیَاتٍ لِّقَوْمٍ یَتَفَکَّرُونَ

Na katika ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo ishara kwa watu wanaofikiri.

 

Familia ambayo ndani yake kuna mapenzi na huruma mapungufu mengi yaliyopo katika familia hiyo hufidiwa, nyoyo za wanafamilia hukurubiana na kwa muktadha huo kupatikana nishati na uchangamfu katika familia. Mtume SAW amenukuliwa akisema: Kila ambaye imani yake ni kamili zaidi, huonyesha mapenzi kwa mkewe. Bwana Mtume SAW alikuwa akiwataka wanaume waamiliane na wake zao kwa mapenzi, huruma na uadilifu. Alikuwa akisema, mtu ambaye ameamua kumuoa mwanamke anapaswa kumthamini na kumuenzi. Imenukuliwa katika kauli yake mashuhuri kwamba:

قَوْلُ الرَّجُلِ لِلْمَرْأَة إِنِّی أُحِبُّکِ، لَا یَذْهَبُ مِنْ قَلْبِهَا أَبَداً

Kauli ya mwanaume kumwambia mwanamke “ninakupenda” katu haiondoki katika moyo wa mwanamke. Aidha historia imenukuu na kuelezea jinsi Bwana Mtume SAW alivyokuwa akimpenda mkewe yaani Bibi Khadija AS. Ukweli huo ulibainishwa na Abu Twalib AS katika hotuba ya akidi aliposema: Khadija na Muhammad wanapendana. Bwana Mtume SAW alikuwa akimuona Bibi Khadija kuwa amekamilisha sifa na hivyo anastahiki kuwa mkewe na daima katika kipindi chao cha maisha ya ndoa, Bwana Mtume SAW alikuwa akiamiliana na Bi Khadija kwa heshima na mapenzi makubwa. Mtume SAW katu hakumlinganisha Bi Khadija na mwanamke yeyote yule.

 

Bwana Mtume SAW analitambua suala la mwanaume kufanya kazi ndani ya nyumba kuwa ni sadaka. Mbora huyo wa viumbe amenukuliwa akimwambia Imam Ali bin Abi Twalib AS:

Ewe Ali kumtumikia mke ni kafara ya madhambi makubwa na kitendo hicho kinashusha ghadhabu za Mwenyezi Mungu. Mtume SAW analitambua suala la mume kutumia muda fulani na kukaa na familia yake ni bora zaidi kuliko kufanya itikafu na ibada katika Msikiti Mtakatifu wa Madina mbora huyo wa viumbe alikuwa akizingatia mno suala la kula chakula pamoja na familia yake na alikuwa akisema, mwanaume yeyote ambaye atatandika kitanga cha chakula na akamtaka mke wake na wanawe waanze kula chakula kwa kutaja jina la Mwenyezi Mungu ‘bismillahi’ na kumaliza kula kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu atawashuhushia rehma na maghufira madhali hawajakunja na kuondoa kitanga chao cha chakula. Tukisoma historia tunakuta kwamba, wakati Bibi Fatma na Ali AS walipomtaka Mtume SAW azigawanye baina yao kazi zao za kila siku Mtume SAW alisema, kazi za ndani atafanya Fatma ma kazi za nje atazifanya Ali.

 

Wapenzi wasikilizaji pamoja na kuwa, kazi za ndani kikawaida zinamhusu mwanamke na kazi za nje ni za mwanaume, hii haina maana kwamba, mwanaume katu hapaswi kumsaidia mkewe kazi za ndani na badala yake na akae tu na kusubiri mkewe afanye kazi zote za ndani na kisha amuandalie kila kitu. Bila shaka kuna wakati mke anahitajia ushirikiano iwe ni wa kikazi au wa kifikra na katika hali kama hii mume anapaswa kumsaidia mkewe.

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki maalumu kilichokujieni kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja ambapo leo tulitupia jicho sehemu tu ya Mtindo wa Maisha ya Bwana Mtume SAW Katika Familia, sina budi kukomea hapa.

Wassalaamu Alaykkum Warahmatullahi Wabarakaatuh

Na Salum Bendera

Tags