Oct 23, 2022 11:27 UTC
  • Tafakuri katika matukio ya hivi karibuni nchini Irani (3- Mipango ya Magharibi ya kuzusha machafuko nchini Irani)

Matukio ya hivi karibuni nchini Iran yamekuwa kisingizio cha nchi za Magharibi kuingilia masuala ya ndani ya Jamhuri ya Kiislamu na kuzidisha au kuchochea machafuko na ghasia.

 Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamekuwa wakitumia nyenzo na fursa zote kwa ajili ya kuiangusha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha miaka 43 iliyopita. Sambamba na sera yao ya kuchafua jina na sura ya Iran (Iran-phobia) katika kanda ya Asia Magharibi na duniani kote, nchi hizo pia zimekuwa zikifanya jitihada kubwa za kuibua machafuko na ghasia ndani ya nchi hii. Mapinduzi ya mahameli na ya rangi bado yapo kwenye ajenda ya Marekani, Canada, Uingereza na baadhi ya nchi nyingine za Ulaya ili kuzusha machafuko nchini Iran. Nchi hizo zimekuwa zikitumia njia zote zinazowezekana kwa ajili ya kuzusha ghasia na machafuko nchini Iran. Madai eti ya kutetea haki za wanawake, haki za binadamu, jinsi ya kufanya uchaguzi, kuzusha shaka katika matokeo ya uchaguzi na jambo lolote linaloweza kuzusha mgawanyiko katika jamii ya Iran au kutumia thitilafu kwa ajili ya kuibua migawanyiko zaidi baina ya wananchi, vyote hivyo vimetumiwa na maadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika miongo michache iliyopita. 

Image Caption

Hakuna shaka kwamba nchi zote za dunia zinakabiliwa na matatizo na masuala na kutoridhika baadhi ya wananchi kuhusu utendaji wa serikali za nchi zao. Nchi zote za kidemokrasia duniani pia zina taratibu za kusimamia matatizo na kushughulikia malalamiko na matakwa ya wananchi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi zenye demokrasia imara zaidi katika eneo hili la Magharibi mwa Asia. Katika mapinduzi yote yaliyofanyika duniani, hakuna sehemu au nchi yoyote iliyoitisha kura ya maoni ya kuainisha aina ya serikali itakayotawala siku hamsini baada ya ushindi wa mapinduzi hayo isipokuwa Iran. Wananchi wa Iran walipiga kura mara tano katika mwaka wa kwanza wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Uchaguzi wa kwanza ulikuwa wa kura ya maoni kuhusu aina ya serikali itakayotawala hapa nchini. Wa pili ulikuwa uchaguzi wa Bunge la Wataalamu wa Katiba, wa tatu ulikuwa kura ya maoni ya rasimu ya katiba. Chaguzi za nne na tano zilizofanyika mwaka wa kwanza baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu zilikuwa za Rais na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran. Katika kipindi chote cha miaka 43 iliyopita ya uhai wa Jamhuri ya Kiislamu kumefanyika zaidi ya chaguzi 40 hapa nchini. Ni katika nchi chache sana za kidemokrasia duniani, ambako kumeshuhudiwa ushiriki mkubwa kama huo wa wananchi katika kuainisha na kuchukua maamuzi juu ya hatima ya nchi yao. Kinyume chake, kuna nchi za kidhalimu na za madikteta wakubwa zaidi duniani zenye mifumo ya kifalme na kikabila katika eneo la Mashariki ya Kati na jirani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na tawala hizo zinaua kwa umati mamia ya maelfu ya wanawake na watoto wa Yemen kwa kutumia ndege na mabomu ziliyopewa na Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi. Mwandishi habari mkosoaji wa utawala huo wa kidikteta alikatwa vipande vipande kwa msumeno na mwili wake ukatupwa kwenye tindikali ili kupoteza ushahidi. Msimamo wa nchi za Magharibi na mashirika ya kimataifa yanayodai kutetea haki za binadamu ulikuwa kunyamaza ukimya mbele ya jinai zote hizi za waziwazi, na mwishowe, ziliamua kutoa taarifa tupu ya kukosoa ukatili na unyama huo ili kujitoa kimasomaso.

Maelfu ya watoto wa Yemen wameuawa katika mashambulizi ya Saudia na washirika wake

Serikali za nchi za Magharibi zinashughulikia matukio ya Iran kwa njia ya kibaguzi na misimamo ya kindumakuwili dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, nchi yenye demokrasia zaidi katika eneo la Magharibi mwa Asia. Nchi hizo, zikishirikiana na tawala fasidi na za kidikteta za kanda hii, zimeanzisha mamia ya vituo vya televisheni, redio na mitandao ya kijamii kama BBC Persian, Manoto na Iran International na kuendesha vita vya kisaikolojia sambamba na njama nyingine nyingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Madhumuni ya vita hivyo ni kuzusha migawanyiko ndani ya taifa la Iran na kuwafanya wananchi wasiwe na imani na serikali na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ili kufikia lengo hilo hutumia njia na wenzo wowote kwa shabaha ya kuzusha ghasia na machafuko hapa nchini. Yaliyojiri hivi majuzi nchini Iran na kifo cha ghafla cha msichana mdogo, Mahsa Amini, yamefanywa kisingizio cha vyombo hivyo vya habari ili kuzusha machafuko nchini, chini ya mwavuli wa kutetea haki za wanawake. Hii ni pamoja na kwamba, ripoti kadhaa, hasa ripoti ya kitaalamu iliyochapishwa kuhusu kifo cha ghafla cha Mahsa Amini, zinaonesha kuwa hakuna dalili za kutendewa ukatili msichana huyo. Uchunguzi wa kitaalamu unaonesha kuwa, Mahsa Amini alikuwa na matatizo ya kiafya ya muda mrefu ambayo yalimsababishia kukosa fahamu na kwa bahati mbaya akafariki dunia akipewa huduma hospitalini.

Sambamba na kifo cha ghafla cha Mahsa Amini ambacho kimetumiwa na nchi za Magharibi na vyombo vyao vya habari kwa ajili ya kuibua machafuko na ghasia nchini na kaunzisha vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran, kulitokea mlipuko wa bomu huko Kabul nchini Afghanistan ulioua makumi ya wasichana na watoto. Hata hivyo hakukushuhudiwa ukosoaji au hata ujumbe wa rambirambi kwa familia za waathithiriwa kutoka kwa nchi za Magharibi na taasisi za kimataifa eti za kutetea haki za binadamu. Kilichojitokeza na kutiwa chumvi zaidi wakati huo katika vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na vibaraka wao kuhusiana na matukio ya wiki za hivi karibuni nchini Iran ni jinsi polisi wanavyokabiliana na waharibifu wa mali za watu na miundombinu ya mijini. Hapana shaka yoyote kwamba, polisi katika eneo au nchi yoyote duniani ambako kundi la watu huingia mitaani na kufanya uharibifu wa mali za umma na taasisi na milki za wananchi, hulazimika kuingilia kati kwa ajili ya kudhibiti na kukomesha uhalifu huo. Kwa mfano tu haipiti siku bila ya walimwengu kushuhudia polisi wakikabiliana na waandamanaji katika mitaa na barabara za miji ya nchi za Magharibi. Hata hivyo pale polisi wa Iran wanapokabiliana na watu wanaofanya ghasia kwa shabaha ya kurejesha nidhamu na utulivu, jambo hilo huonekana kama kioja na kinyume cha sheria! Ni vyema kukumbusha hapa pia kwamba, polisi kadhaa wameuawa katika matukio ya hivi karibuni hapa nchini wakiwa katika jitihada za kurejesha amani na utulivu, lakini hakuna chombo chochote cha habari cha nchi za Magharibi kilichoashiri suala hilo.

Polisi kadhaa wa Iran wameuawa katika machafuko ya karibuni hapa nchini

Mienendo hiyo ya kinafiki na kindumakuwili ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, Uingereza na Canada kuhusiana na matukio yaliyojiri Iran ni kielelezo cha njama na mipango ya nchi za Magharibi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Vilevile nara zinazopigwa na wafanyaghasia katika baadhi ya mitaa ya Iran chini ya uongozi wa vyombo vya habari vya nchi za Magharibi, ni ishara tosha ya lengo lao la kuibua hali ya kutoaminiana kati ya wananchi na serikali, na kuzusha mgawanyiko kati ya wananchi wa Iran. Aidha kuhuishwa makundi ya kigaidi ndani na katika nchi jirani na Iran hususan Kurdistan ya Iraq na huko Pakistan, kunaonyesha kuwa, nchi za Magharibi bado zina matumaini ya kuuangamiza mti imara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa hatua hizo za vita vya kisaikolojia na kwa kuyaunga mkono magenge ya kigaidi. Huko Zahedan, makao makuu ya mkoa wa Sistan na Baluchestan, kundi moja la kigaidi lilishambulia kituo cha polisi na kuua makumi ya watu, wakiwemo polisi kadhaa. Vyombo vya habari vya Magharibi vililitaja tukio hili kuwa ni maandamano ya kutetea haki za wanawake! ilihali mkono wa makundi ya kigaidi yenye silaha zilizopatikana kutoka kwao ulishuhudiwa waziwazi katika matukio ya umwagaji damu ya mji wa Zahedan.

Katika mkoa wa Kurdistan, makundi ya kigaidi ambayo mikono yao imetapakaa damu ya maelfu ya wanawake na watoto na maafisa wa polisi katika miongo minne iliyopita, yalijaribu kutumia fursa hiyo ili kuzusha machafuko na ghasia nchini Iran. Miongoni mwa makundi hayo ya kigaidi ni yale ya PJAK, na Komala. Makundi haya yamefanya jinai na uhalifu wote wa kutisha dhidi ya raia na maafisa wa usalama wa Iran katika kipindi chote cha zaidi ya miongo minne iliyopita. Makundi yote hayo ya kigaidi yanaungwa mkono na serikali za nchi za Magharibi na yana ofisi na shughuli rasmi katika nchi hizo. Hata hivyo, kwa kuwa makundi hayo ya kigaidi yamesimama dhidi ya Iran ya Kiislamu, serikali za nchi za Magharibi zinayaunga mkono kwa hali na mali ili kuibua mgogoro nchini Iran.

Pamoja na hayo yote, Mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyofanywa hivi karibuni na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya makao makuu ya makundi ya kigaidi huko Kurdistan nchini Iraq, yameudhihirishia ulimwengu mzima kwamba, jeshi hilo halitakaa kimya katika kukabiliana na kitendo chochote cha kuzusha ghasia na mgogoro na cha kigaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika hotuba yake ya siku chache zilizopita kwenye kikao cha washiriki kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu mjini Tehran kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume Muhammad (saw), Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alisema: “Tulisimama kidete mbele ya madola makubwa. Wakati mmoja, dunia hii ilikuwa mikononi mwa madola makubwa mawili: Dola la Marekani na lile la Muungano wa Sovieti. Madola yote hayo mawili ambayo yalikuwa yakitofautiana katika masuala mengi, yalikubaliana na kuafikia katika suala moja ambalo ni kuipiga vita Jamhuri ya Kiislamu. Walidhani kwamba wangeweza kung'oa mche huo. Hata hivyo hii leo, mche huo umekuwa mti imara na madhubuti."

Ayatullah Ali Khamenei

 

Tags