Palmyra, Lulu ya Jangwani, kabla na baada ya kuhujumiwa na ISIS
Jeshi la Syria hivi karibuni liliukomboa mji wa kale wa Palmyra au Tadmur kutoka kwa kundi la magaidi wakufurishaji wa ISIS au Daesh. Makala yetu ya leo itaangazia kwa kifupi kuhusu mji huo muhimu na wa kihistoria nchini Syria
Mji wa Palmyra ulikaliwa kwa mabavu na magaidi wa ISIS mwezi Juni mwaka 2015. Baada ya miezi kadhaa ya jitihada za jeshi la Syria mji huo ulikombolewa na jeshi hilo mwishoni mwa mwezi Machi.
Katika kipindi cha kukaliwa kwa mabavu mji huo, mamia ya wakaazi wake waliuawa na magaidi wakufurishaji wa ISIS. Aidha magaidi wa ISIS mbali na ukatili wao pia waliharibu majengo ya kihistoria ya mji huo. Mji wa Palmyra ulikuwa na mabaki ya majengo ya historia adhimu ya miaka 2,000 lakini baada ya kutekwa na ISIS mabaki mengi ya mji huo yaliporwa au kuharibiwa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), na taasisi zingine za kimataifa zilikuwa kimya kuhusu mauaji ya watu wa Syria kabla ya kutekwa mji wa Palmyra. Lakini baada ya kutekwa mji huo wa kale mashirika hayo yalibainisha wasi wasi wao kwa ajili tu ya majengo ya kihistoria katika mji huo!!
Wakati walipokuwa wanaushikilia mji huo, magaidi wa ISIS walitumia mabaki ya ukumbi wa kale wa mji huo kuwaua kinyama wapinzani wao. Aidha walimpiga risasi na kumuua Khaled Mohamad al-Asaad mtaalamu wa mambo ya kale na mkuu wa zamani wa turathi za kale mjini Palmyra. Al-Asaad, aliyekuwa na umri wa miaka 81, aliuawa na magaidi wa ISIS baada ya kukataa kuwaonyesha alikokuwa ameficha turathi za kale. Katika kueneza uharibifu wao, magaidi wa ISIS waliharibu mahekalu ya kale yaliyojengwa zaidi ya miaka 2000 ya Baal Shamin na Bel. Aidha waliharibu makaburi kadhaa ya kale mjini humo.
Kabla ya kuanza hujuma dhidi ya Syria mwaka 2011, sekta ya utalii ilikuwa moja kati ya nguzo muhimu za kiuchumi nchini humo. Idadi kubwa ya Wasyria walikuwa wakifanya kazi katika sekta hiyo au sekta zingine zinazofungamana na sekta hiyo. Aidha kabla ya vita vya ndani Syria watalii zaidi ya laki moja na nusu wa kigeni walikuwa wakiutembelea mji wa Palmyra. Lakini baada ya miaka kadhaa ya vita na umwagaji damu, Syria sasa haina pato lolote kutokana na utalii na tunaweza kusema hakuna mtalii anayetembelea nchi hiyo kwa sasa.
Mbali na masikitiko na majonzi makubwa walio nayo wapenda uhuru duniani kuhusu idadi kubwa ya watu waliouawa kutokana na ukatili wa magaidi wanaopata himaya ya kigeni Syria, pia watu wengi wameumwa sana na magaidi hao kuharibu turathi za kale za nchi hiyo ya Kiarabu. Mbali na Palmyra, magaidi pia wameharibu na kubomoa maeneo ya kihistoria katika miji wa Damascus, Halab, Basri na eneo la kihistoria la kaskazini mwa Syria lijulikanalo kama Al Mudun al Mayyit au 'Miji ya Wafu' . Hali kadhalika magaidi wa ISIS wamekuwa wakitekeleza hujuma za mara kwa mara dhidi ya Haram Takatifu ya Bibi Zainab SA, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW. Aidha magaidi hao wakufurishaji wa Kiwahhabi wamebomoa maeneo mengine mengi yanayoenziwa na kuheshimuwa na Waislamu nchini Syria. Ni jambo la kusikitisha kuwa magaidi nchini Syria wangali wanaendeleza ukatili na uharibifu wao. Tokea kuanza hujuma zao Syria magaidi wa ISIS pia wamebomoa kikamilifu makaburi na maziara ya masahaba watukufu wa Mtume wa Uislamu SAW kama vile Uwais al-Qarani , Ammar ibn Yasir na Ubay ibn Qais al-Nakha'i. Fauka ya hayo kundi linalojiita Jeshi Huru la Syria, pia lilibomoa kaburi la mjini Damascus la Hujr ibn 'Adi al-Kindi shakhsia maarufu wa zama za kudhihiri Uislamu.
Kimsingi ni kuwa magaidi wa Kiwahhabi mbali na kuua malaki ya raia wa Syria pia wametekeleza uharibifu mkubwa wa turathi za kale za nchi hiyo. Ingawa magaidi hao wanadai wana malengo ya kidini lakini ukweli ni kuwa vitendo vyao viko mbali na nje kabisa ya mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu bali hata pia hawafungamani hata kidogo na ubinadamu. Miaka miwili iliyopita mmoja kati ya vinara wa kundi la kigaidi la ISIS nchini Syria alitangaza kuwa makanisha yote yaliyiojengwa baada ya kudhihiri Uislamu yanapaswa kubomolewa. Jambo hilo linaonyesha kuwa magaidi hao si tu kuwa wana taasubi na fikra zilizoganda bali pia wanataka kuibua malumbano ya kidini na kuwagonganisha wafuasi wa dini mbali mbali. Hii ni kwa sababu Mtume Mktukufu wa Uislamu SAW hakuwahi kutumia mbinu ya kubomoa maeneo ya ibada ya wafuasi wa dini za mbinguni.
Damascus, mji mkuu wa Syria, pia ni maarufu kama kama 'Lango la Historia'. Mji huo ni kati ya miji ya kale zaidi duniani na wanadamu walikuwa wanaishi mjini humo takribani miaka elfu kumi kabla ya Milladia. Ni kwa msingi huo ndipo mji wa Damascus ukatajwa kuwa 'Mji Mkuu wa Kwanza Duniani'.
Mji wa Damascus umeshuhudia kuibuka na kuenea staarabu za kale zaidi za mwanadamu ambazo ziliibuka katika ardhi za mashariki mwa dunia. Mji huu umewahi kuwa mji mkuu wa zama mbali mbali za tawala au falme katika historia. Mwaka 636 Miladia mji wa Damascus ulitangazwa kuwa mji mkuu wa Ulimwengu wa Kiislamu na hivyo ukawa mji muhimu zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu. Mji huo ulifanywa makao ya Khilafa ya Bani Umayya na hivyo uliweza kunawiri katika kipindi hicho. Mji wa Damascus umekuwa sehemu ya kuzaliwa mitume, watu wakubwa katika historia, wasomi, wanafirka, malenga, wanafalaki, wanazuoni, n.k ambao wote wamekuwa na nafasi muhimu katika kustawi dini, utamaduni, elimu na kuenea dini mbali mbali.
Mji wa Palmyra au Tadmur ni moja kati ya miji ya kale ya Syria na uko katika mkoa wa Homs. Katika zama za utawala wa Wahellen (Hellenic ) na Wabyzantine (Byzantine ) mji huo ulikuwa kati ya vituo muhimu vya ustaarabu ambapo kulikuwa na usanifu majengo maridadi na wa kustaajabisha na hivyo kuupa mji huo utambulisho wa kipekee. Katika historia, wakaazi wa Palmyra walikuwa ni kutoka kaumu za Waamori (Amorites), Waaramia (Arameans) na Waarabu pamoja na idadi ndogo ya ya Mayahudi. Mwaka 1932 baada ya kuanza utafiti katika magofu ya mji wa kale wa Palmyra, waliokuwa wakiishi hapo walihamishiwa mji mpya wa Palmyra. Kwa hakika eneo la Palmyra ni mchanganyiko wa tamaduni za Waplmyra, Waashkani (Askhanian) na Wagiriki au Wayunani. Mji huu wa kale ambao ni maarufu kama 'Lulu ya Jangwani' ni moja kati ya magofu muhimu zaidi ya kihistoria duniani na ni kati ya turathi za dunia zilizo katika orodha ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Historia ya magofu adhimu ya Palmyra inarejea nyuma katika kipindi cha zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita.
Katika zama za kale, mji wa Palmyra ulikuwa moja ya vituo muhimu zaidi vya utamaduni duniani. Mji huu ni kielelezo cha sanaa na usanifu majengo bora wa zama zake ambapo kulitumika mbinu za Kiroma na Kigiriki ambazo zilichanganywa na ujuzi na uwezo wa watu wa eneo hilo la kale. Aidha ushawishi wa Iran ya kale uko wazi katika mji huo. Magofu ya Palmyra yana eneo lenye nguzo zaidi ya elfu moja pamoja na eneo lenye makaburi ya kale zaidi ya 500.
Mji wa Palmyra awali ulijengwa na Waashkani (Ashkanids) wakati wa utawala wao mpana uliofika hadi katika eneo la Sham. Lakini baada ya muda usio mrefu, kufuatia hujuma ya Warumi ardhi hiyo iliondoka nje ya duara la utawala wa Iran na ikadhibitiwa na Warumi. Baada ya hapo mji huo ukawa mji mkuu wa Malikia Zenobia wa Syria. Palmyra au Tadmur ni mji maridadi wenye nguzo zenye rangi ya dhahabu yenye kupendeza. Mji huo ulikuwa kituo muhimu zaidi cha biashara baina ya Asia na Ulaya katika karne ya kwanza kabla ya Miladia. Hatimye mwaka 274 Miladia mji huo ulibomolewa katika hujuma ya Mfalme Aurelian wa Roma. Mji huu wa kale una maeneo kadhaa kama vile, ngome ya Palmyra, Hekalu ya Baal na Lango la Hadrian.
Agosti 23 mwaka 2015 Shirika la UNESCO lilitangaza kuwa magaidi wa ISIS walibomoa hekalu la Baal Shamin kwa kutumia mabomu. Hekalu hilo lilijengwa karne ya kwanza Miladia.
Palmyra ni mji ambao umeathiriwa sana na ujenzi uliokuwa katika miji ya Ugiriki na Roma. Medani zenye nguzo ndefu, chemichemi za maji, viwanja vya tamthilia ni mifano ya mbinu za usanifu majengo za Ugiriki zipatikanazo Palmyra.
Tokea mji huo ukaliwe kwa mabavu na ISIS, kulijiri mauaji ya kinyama ya wakaazi wake pamoja na kuuawa pia idadi kubwa ya wasomi bingwa wa historia mbali na kuharibiwa turathi zake za kale.
Mkuu wa Turathi za Kale Syria, Bw. Abdulkarim alibainisha masikitiko yake mwezi Juni mwaka jana baada ya magaidi wa ISIS kuharibu kinyango cha kihistoria kijulikanacho kama Simba wa Al-lāt. Pamoja na jinai na uharibifu mkubwa uliotekelezwa na magaidi wakufurishaji wa Kiwahhabi, tarehe 27 Machi mwaka 2016, mji wa Palmyra ulikombolewa na kudhibitiwa kikamilifu na Jeshi la Syria. Baada ya kuteguliwa mabomu yaliyokuwa yametegwa jeshi hilo liliwatimua kikamilifu magaidi wa ISIS mjini humo. Lakini la kusikitisha ni kuwa, picha na taswira kutoka mji huo zinaonyesha kuharibiwa au kubomolewa majengo na magofu ya kale na hivyo adhama ya lulu hii ya jangwa imedidimia.