Aug 01, 2021 02:26 UTC
  • Kuendelea mashambulizi ya Daesh huko Iraq katika kufanikisha njama za Wamarekani

Vyombo vya habari vya Iraq Ijumaa usiku vilitangaza kuwa kundi la kigaidi la Daesh lilishambulia shuguli ya mazishi katika mji wa Yathrib kusini mwa mkoa wa Salahuddin huko kaskazini mwa Iraq. Watu saba wameuawa na wengine 17 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la Daesh.

Baada ya shambulio hilo jeshi la Iraq lilianzisha oparesheni ya kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika wa hujuma hiyo ya kigaidi huku kundi la wapiganaji wa Hashdu Shaabi likitoa taarifa na kutangaza kuwa, tayari limetuma wapiganaji na zana za kijeshi katika eneo palipojiri shambulio la kigaidi kwa ajili ya kuvisadia vikosi vya usalama. Kuna nukta muhimu hapa za kuashiria kuhusu kitendo hicho cha kigaidi cha Daesh. 

Ya kwanza ni kuwa, licha ya kushindwa vibaya kundi la Daesh huko Iraq, mamluki wa kundi hilo wangali katika maeneo mbalimbali nchini humo na wanafanya hujuma na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya wananchi na taasisi za serikali za nchi hiyo. 

Nukta ya pili, kundi la wapiganaji wa kujitolea la wananchi wa Iraq la Hashdu Shaabi ni nguzo muhimu ya mapambano dhidi ya makundi ya kigaidi na limekuwa likiwalinda wananchi na taasisi za serikali ya Iraq licha mashambulizi makubwa ya kipropaganda na ya kulipata matope kundi hilo yanayofanywa na baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na kikanda. Kwa msingi huo, kundi la Hashdu Shaabi linahesabiwa kuwa tegemeo kuu la wananchi wa Iraq. 

Wapiganaji wa al Hashdu Shaabi

Nukta ya tatu ni kwamba kuibuka tena kwa kundi la Daesh na kuendelea harakati za kundi hilo likiwa limejizatiti kwa zana za kivita ni ushahidi tosha wa namna baadhi ya nchi za kieneo na kimataifa zinavyoliunga mkono kwa hali na mali kundi hilo la kigaidi. Kwa maneno mengini ni kuwa, kundi hilo la kigaidi linaendelea kutumiwa kama wenzo wa kuzusha machafuko na hali ya mchafukoge huko Iraq; na pale inapolazimu wafadhili wa Daesh huwahamisha wanachama wa kundi hilo katika maeneo mbalimbali ya Iraq na au huwaondoa nchini humo na kuwahamishia katika nchi nyingine.  

Nukta ya nne inahusu udharura wa kuondoka wanajeshi vamizi wa Marekani katika nchi za eneo la Magharibi mwa Asia ikiwemo Iraq. Mustafa al Kadhimi Waziri Mkuu wa Iraq ametangaza katika safari yake ya karibuni nchini Marekani kwamba, wanajeshi wa Marekani watakuwa wamerejea nchini kwao hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Inaonekana kuwa, msimamo huo wa Marekani ni matokeo ya baadhi ya mashinikizo yaliyopo nchini humo dhidi ya Washington na serikali ya Iraq; kwa maneno mengine ni kwamba, Marekani inafanya kila linalowezekana kumpunguzia al Kadhim mzigo wa mashinikizo katika wakati huu wa kukaribia kufanyika uchaguzi mkuu nchini Iraq. Kwa msingi huo, kadiri muda wa uchaguzi huo unavyokaribia tunapasa kutarajia ongezeko la mashambulizi ya kigaidi nchini Iraq ambayo yatatumiwa na Marekani kama kisingizio tosha cha kubakisha wanajeshi wake nchini Iraq kinyume na agizo la Bunge la nchi hiyo lililotaka kuondoka wanajeshi wote wa nchi za kigeni katika ardhi ya Iraq.  

Bunge la Iraq

Nukta ya tano ni kwamba, kuendelea mashambulizi ya kigaidi huko Iraq ambayo yamepamba moto katika siku za karibuni, kunafungamana na suala la kukaribia uchaguzi wa Bunge la nchi hiyo. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika tarehe 10 Oktoba mwaka huu. Inaonekana kuwa mashambulizi hayo ya kigaidi yanafanyika kwa malengo mawili: 

Kwanza ni kutaka kuakhirisha uchaguzi wa Bunge wa nchi hiyo kwa kisingizio kwamba hakuna usalama wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya makundi na vyama vya Iraq ukiwemo Muungano wa al Saairun unaoongozwa na Muqtada Sadr vimetangaza kuwa havitashiriki katika uchaguzi huo ili kutoa fursa zaidi kswa makundi yanayoungwa mkono na Marekani.

Pili ni jitihada za kuchafua jina la kundi la wapiganaji wa kujitolea la al Hashdu Shaabi nchini Iraq na kutumia anga ya ukosefu wa amani kulipaka matope kundi hilo na vyama vingine vya siasa vinavyounga mkono kambi ya mapambano dhidi ya Marekani na washirika wake. Njama hiyo ina shabaha ya kulidhihirisha kundi hilo la wananchi kuwa limefeli na kushindwa.