Mapigano makali yanaendelea katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum
Sep 16, 2023 07:16 UTC
Duru za habari nchini Sudan zimeripoti kuwa, mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya Jeshi na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, RSF.
Mashuhuda mjini Khartoum wameripoti leo kuwa, mapigano makali yametokea karibu na makao makuu ya jeshi yaliyoko katika mji mkuu huo wa Sudan.
Imeelezwa kuwa kila aina ya silaha imetumiwa katika mapigano hayo.
Jeshi la Sudan limetangaza kuwa, katika mji wa Omdurman ulioko magharibi mwa Khartoum, limewakabidhi kwa wawakilishi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu vijana chipukizi 30 waliokuwa wamekamatwa mateka na vikosi vya jeshi hilo katika mapigano na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka.
Taarifa ya jeshi la Sudan imeeleza kwamba wawakilishi wa Msalaba Mwekundu watawakabidhi vijana hao kwa familia zao.
Wakati huo huo, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan (UNITAMS) umetangaza kuwa umefanya mazungumzo na mashauriano na jeshi na vikosi vya RSF ili kuzishawishi pande hizo mbili zisitishe mapigano.
Mapigano ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya Jeshi na vya usaidizi wa haraka RSF, chanzo kikiwa ni ugomvi wa kuwania madaraka; na juhudi za upatanishi wa kimataifa za kukomesha mapigano hayo kwa kuzileta pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa hazijazaa matunda.
Usitishaji vita umeshatangazwa mara kadhaa nchini Sudan kupitia upatanishi huo wa kimataifa, lakini umekuwa ukikiukwa na pande zinazopigana.
Vita hivyo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 5,000 wengi wao wakiwa raia, na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa. Wasudan wengine zaidi ya milioni tano wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.../
Tags