UN yashtushwa na vifo vya watoto katika kambi za wakimbizi Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i102434-un_yashtushwa_na_vifo_vya_watoto_katika_kambi_za_wakimbizi_sudan
Umoja wa Mataifa umesema watoto zaidi ya 1,200 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa surua na utapiamlo katika kambi za wakimbizi nchini Sudan.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 19, 2023 22:53 UTC
  • UN yashtushwa na vifo vya watoto katika kambi za wakimbizi Sudan

Umoja wa Mataifa umesema watoto zaidi ya 1,200 wameaga dunia kutokana na ugonjwa wa surua na utapiamlo katika kambi za wakimbizi nchini Sudan.

UN ilisema hayo jana Jumanne na kutoa indhari kwamba, maelfu ya watoto wengine wakiwemo wa kuzaliwa wapo katika hatari ya kupoteza maisha kufikia mwishoni mwa mwaka huu, iwapo hatua za dharura za kunusuru maisha ya watoto hao walioko kambini hazitachukuliwa.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza kwamba maelfu ya watoto wa Sudan wanahitaji msaada wa dola milioni 400 ili waweze kubakia hai.

Kadhalika Shirika la Save the Children lilisema katika taarifa yake ya karibuni kwamba, tangu mwezi Aprili mwaka huu mpaka sasa, kwa uchache watoto 498, na pengine mamia zaidi, wamefariki dunia kwa njaa nchini Sudan.

Hii ni katika hali ambayo, mapigano makali yanaendelea kati ya vikosi vya Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF hasa katika mji mkuu Khartoum.

Mapigano Sudan

Mapigano hayo ya silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 mwaka huu, chanzo kikiwa ni ugomvi wa kuwania madaraka; na juhudi za upatanishi wa kimataifa za kukomesha mapigano hayo kwa kuzileta pande hizo mbili kwenye meza ya mazungumzo hadi sasa hazijazaa matunda.

Vita hivyo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 5,000 wengi wao wakiwa raia, na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa. Wasudan wengine zaidi ya milioni tano wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.