Al-Burhan: Vita vya Sudan huenda vikaenea Afrika Mashariki
Jenerali Abdul Fattah al-Burhan, mkuu wa baraza la uongozi la Sudan ameuonya Umoja wa Mataifa kuwa, vita vinavyoendelea kushuhudiwa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika yumkini vitatanuka zaidi na kuenea katika nchi za Afrika Mashariki.
Al-Burhan alitoa indhari hiyo katika hotuba yake mbele ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kuongeza kuwa, "Hatari ya vita hivi sasa ni tishio kwa amani na usalama wa kieneo na kimataifa. Waasi hao (wa RSF) wametafuta uungaji mkono kutoka kwa makundi haramu na ya kigaidi kutoka nchi mbalimbali za kieneo na kote duniani kwa ujumla."
Mapigano hayo ambayo yametawanyika katika maeneo tofauti ya Sudan, yakijikita zaidi katika mji mkuu Khartoum yangali yanaendelea huku maelfu ya raia wakiuawa au kujeruhiwa.
Mkuu wa baraza la uongozi la Sudan ametoa mwito wa kuwajibishwa na kufikishwa mbele ya sheria makundi ya mamluki yanayounga mkono na kuchochea vita vya Sudan.
Amesema Sudan inaendelea kushuhudia idadi ya kutisha ya mauaji, ubakaji, watu kufurushwa makwao, magendo ya mihadarati na hata watoto kusajiliwa kujiunga na makundi hayo.
Siku ya Jumatano, mkutano maalumu wa serikali na mashirika ya kimataifa ili kujadili mgogoro unaonedelea sasa nchini Sudan ulifanyika pembeni ya Kikao cha 78 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mjini New York.
Mapigano ya utumiaji silaha nchini Sudan yalianza Aprili 15 kati ya vikosi vya jeshi na vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa lengo la kuwania madaraka, na usuluhishi wa kimataifa uliofanywa kwa madhumuni ya kuhitimisha mapigano hayo na kuzikutanisha pande mbili kwenye meza ya mazungumzo haujazaa matunda hadi sasa.
Kwa mujibu wa Asasi Isiyo ya Kiserikali ya Acled, vita hivyo vimesababisha vifo vya watu wasiopungua 7,500 wengi wao wakiwa raia, na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa. Wasudan wengine zaidi ya milioni tano wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na mapigano hayo.