Kufikia kikomo uwepo wa kijeshi wa Ufaransa nchini Niger; ushindi kwa Waniger
(last modified Sun, 24 Dec 2023 11:10:02 GMT )
Dec 24, 2023 11:10 UTC
  • Kufikia kikomo uwepo wa kijeshi wa Ufaransa nchini Niger; ushindi kwa Waniger

Miezi kadhaa baada ya kutokea mabadiliko ya kisiasa nchini Niger na sisitizo la Baraza la Kijeshi la kuondoka vikosi vya kijeshi vya Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo, hatimaye kundi la mwisho la askari wa Paris liliondoka Niger siku chache zilizopita.

Kuondoka kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa kulifanyika Ijumaa katika hafla iliyohudhuriwa na makamanda wakuu wa jeshi la Niger katika Kituo cha Anga cha 110 cha Niamey. Kwa kuondoka kundi hilo la wanajeshi wa Ufaransa mjini Niamey, uwepo wa kijeshi wa Ufaransa huko Niger umefikia kikomo.

Kuondoka nchini Niger kundi la mwisho la askari wa Ufaransa

Kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa nchini Niger kumetimia wakati vikosi vya nchi hiyo ya Magharibi vimekuwepo moja kwa moja au njia isiyo ya moja kwa moja na kwa miongo kadhaa katika nchi mbalimbali za Afrika, hasa za Jumuiya ya Sahel.

Kwa hakika, Ufaransa ambayo ililazimika kusitisha uwepo wake rasmi wa kijeshi katika nchi nyingi za bara hilo kufuatia harakati za kupigania ukombozi katika nchi mbalimbali za Kiafrika katika miongo kadhaa iliyopita, katika miaka ya karibuni ilitumia mbinu mpya za ukoloni mamboleo kurejea na kujizatiti tena katika nchi hizo.

Madai ya kupambana na ugaidi na kuzisaidia nchi za Afrika kujiendeleza kiustawi na kidemokrasia ni miongoni mwa mbinu zilizotumiwa na Ufaransa kurejea katika nchi za Afrika.

Kwa mtazamo wa kiuchumi na kibiashara, mashirika mbalimbali ya Ufaransa yamekuwa yakiwekeza katika miradi ya kiuchumi na migodi katika nchi za Afrika kwa miaka mingi. Mingi ya miradi hiyo imekuwa ikitekelezwa kupitia mikopo ya muda mrefu.

Ingawa kidhahiri miradi hiyo imekuwa ikitekelezwa kwa madai ya ushirikiano wa kiuchumi, lakini ukweli wa mambo ni kuwa Ufaransa imekuwa ikimiliki sehemu kubwa ya hisa za migodi na mashirika ya madini katika nchi hizo na hivyo kuathiri moja kwa moja uchumi wa nchi hizo. La msingi ni kwamba Ufaransa imekuwa ikifuatilia kudhamini maslahi yake binafsi ya kiuchumi katika nhi nyingi za Kiafrika ambapo kwa mfano imekuwa ikijidhaminia zaidi ya asilimia 20 ya mahitaji yake ya madini ya urani kutoka Niger.

Katika upande mwingine na katika muongo mmoja uliopita, Ufaransa imetuma wanajeshi wake katika nchi mbalimbali za bara hilo hususan Mali na Niger kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Licha ya madai hayo ya Paris, vikosi hivyo vya kigeni si tu havijafanya lolote la maana katika kuyatokomeza makundi ya kigaidi, bali vimefanya mambo mengi yaliyo kinyume cha sheria ambayo yamezikasirisha nchi za Kiafrika.

Mauaji ya kihalifu dhidi ya raia, ubakaji, mauaji na kugunduliwa makaburi ya umati karibu na kambi za wanajeshi wa Ufaransa ni baadhi ya mambo ambayo yamepelekea raia wa nchi za Kiafrika kutaka kuondolewa mara moja askari hao katika nchi zao. Kama tulivyoshuhudia katika miezi kadhaa iliyopita, mapinduzi ya kijeshi katika nchi za Mali, Burkina Faso na Niger yalikaribishwa na kuungwa mkono pakubwa na raia wa nchi hizo ambazo viongozi wao walikuwa vibaraka wa Ufaransa.

Hata kama kufuatia mapinduzi hayo, Ufaransa bado ilitarajia kuwa ingeweza kudumisha uwepo wake katika nchi hizo, lakini kutokana na uungaji mkono mkubwa wa watu wa nchi hizo kwa mabadiliko ya kisiasa na viongozi wapya wa kijeshi, Ufaransa na washirika wake walishindwa kudumisha uwepo wao katika nchi hizo kwa sababu takwa la kwanza la serikali mpya za kijeshi lilikuwa ni kufukuzwa askari wa Ufaransa katika nchi hizo.

Watu wa Niger wakiandamana dhidi ya uwepo wa kijeshi wa Ufaransa

Katika miezi ya hivi karibuni, serikali ya kijeshi ya Niger na watu wa nchi hiyo pia wamekuwa wakisisitiza sana juu ya kudumishwa umoja wa ardhi na kujitawala kisiasa na kiuchumi nchi yao. Ni kutokana na ukweli huo ndipo viongozi wa Baraza la Kijeshi wakawataka rasmi Wafaransa waondoke.

Kufuatia mashinikizo makubwa yaliyotolewa na serikali mpya za Mali, Burkina Faso na sasa Niger, serikali ya Ufaransa hatimaye imelazimika kuwaondoa askari wake wote katika nchi za eneo la Sahel.

Kufuatia tukio hilo muhimu la kufukuzwa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi zilizotajwa, Baraza la Kijeshi la Niger limetaja tukio hilo kuwa mwanzo wa "zama mpya" kwa watu wa Niger. Baraza hilo lilichapisha chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X likisema: "Niger bado imesimama imara na usalama wa ardhi yetu hautategemea tena uwepo wa wageni. Tumedhamiria kukabiliana na changamoto zinazotukabili kwa kuimarisha uwezo wetu wa kistratijia na kijeshi wa taifa."