Jul 06, 2016 04:31 UTC
  • Waasi wa ADF waua watu 9 kaskazini mwa Kongo DR

Watu 9 wameuawa na kundi la waasi wa ADF-Nalu wa Uganda kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mak Hazukay, msemaji wa serikali katika mkoa wa Beni amesema waasi wa ADF-Nalu jana Jumanne walishambulia kijiji cha Oicha, kaskazini mashariki mwa nchi na kuua wanakijiji 9 wakiwemo wanawake watano.

Hivi karibuni jeshi la Kongo DR lilianzisha operesheni kubwa dhidi ya waasi hao wa Uganda walioko katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa nchi hiyo.

Mwezi Mei mwaka huu, kundi la waasi wa ADF-Nalu lilifanya mashambulio katika mkoa wa Ituri huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuuwa watu kadhaa.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likikumbwa na machafuko kwa zaidi ya miaka 20 sasa kutokana na kuwa ngome ya makundi kadhaa ya waasi kutoka nchi jirani za Rwanda na Uganda.

Baadhi ya vijiji vya mashariki mwa nchi hiyo vinadhibitiwa na makundi ya waasi hali ambayo imewafanya wakazi wake kuyaacha makazi yao na kuwa wakimbizi.

Tags