EU yayawekea vikwazo makampuni sita yanayodaiwa kuhusika katika kufadhili vita Sudan
Baraza la Ulaya limeidhinisha vikwazo kwa makampuni sita yanayodaiwa kuhusika katika kufadhili vita nchini Sudan, ambapo vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo (SAF) na Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wamekuwa wakipigana tangu Aprili mwaka jana.
Baraza la Ulaya lilisema jana Jumatatu kuwa taasisi hizo sita zimehusika kufadhili shughuli na vitendo vinavyodhoofisha usalama na utulivu wa kisiasa huko Sudan. Miongoni mwa taasisi zilizotajwa na Baraza la Ulaya ni makampuni mawili yanayojihusisha na utengenezaji wa silaha na magari kwa ajili ya SAF (Defense Industries System na SMT Engineering); Kampuni ya Zadna International for Investment Limited inayodhibitiwa na jeshi la jeshi la Sudan na kampuni tatu zilizohusika katika ununuzi wa vifaa vya kijeshi kwa ajili ya Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) yaani (Al Junaid Multi Activities Co Ltd, Tradive General Trading na GSK Advance Company Ltd).
Taarifa ya Baraza la Ulaya imebainisha kuwa: Umwagaji damu umeendelea kuongezeka huko Sudan licha ya juhudi za jamii ya kimataifa ili kusitishwa mapigano nchini humo. Raia wa Sudan wasiopungua milioni 7.5 wamelazimika kuyahama makazi yao kufuatia vita vilivyoikumba nchi hiyo.