Mar 22, 2024 06:58 UTC
  • Mgomo wa madaktari nchini Kenya umeingia wiki ya pili huku huduma za dharura zikisitishwa

Madaktari nchini Kenya wamesitisha kutoa huduma za dharura katika hospitali za serikali na hivyo kuutumbukiza mfumo wa afya katika mgogoro mkubwa zaidi huku mgomo wa kitaifa wa madaktari ukiingia wiki ya pili jana Alhamisi.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU), Davji Atella amesema kuwa muungano huo unasimama kidete katika uamuzi wake wa kusitisha hata huduma za dharura za kimsingi hospitalini.

David Atella

Atella ameliambia shirika la habari la Anadolu kwamba, wameamua kuwa hata huduma za chini kabisa za dharura zilizokuwa zikitolewa kwenye baadhi ya hospitali za rufaa sasa zimefungwa, na huo ndio ukweli.' 

Amesema, wataendelea na msimamo wao huo hadi pale serikali itakaposhughulikia suala la kuachishwa kazi madaktari, jambo ambalo ni muhimu kwa muungano katika mazungumzo.

Mgomo huu wa sekta ya afya Kenya ambao jana uliingia katika wiki ya pili umesababisha wagonjwa kukosa huduma muhimu za matibabu, jambo ambalo limezua wasiwasi mkubwa kote nchini humo huku maelfu ya madaktari wakisusia kuripoti hospitalini.

Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya (KMPDU) umechukua uamuzi wa kusitisha huduma za dharura  huku madaktari wakiitaka serikali kushughulikia malalamiko yao hasa kuhusu ucheleweshaji wa kuajiri wahudumu wa afya.

Tags