Mar 28, 2024 02:28 UTC
  • Kenya kujenga kituo cha nyuklia cha utafiti chenye kugharimu dola milioni 83

Kenya itahitaji angalau Shilingi bilioni 11 (takribani dola milioni 83) kama gharama ya awali ya kutengeneza kinu cha kwanza cha utafiti wa nyuklia nchini humo katika kile kinachotarajiwa kuwa hatua ya kuelekea katika uzalishaji wa nishati ya nyuklia siku zijazo.

Vinu vya utafiti ni vinu vya nyuklia vinavyotumika kwa utafiti, elimu na mafunzo.

Wakala wa Nishati na Nishati ya Nyuklia Kenya (NuPEA), wakala wa Serikali unaoongoza mpango wa nishati ya nyuklia katika nchi hiyo, unasema kuwa utaomba kiasi hicho kutoka kwa Hazina katika awamu mbili kusaidia kufikia asilimia 40 ya gharama za awali za mradi wa nyuklia wa Kenya.

Wakala wa Nishati na Nishati ya Nyuklia Kenya unahitaji dola milioni 22.7 mwaka wa 2026 na milioni 60 milioni 2027 kwa ajili ya mradi huo, ambayo inatazamiwa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi. Shirika hilo linasema katika mpango wa kimkakati uliozinduliwa hivi majuzi wa 2023-2027 kwamba, kinu hicho cha nyuklia cha utafiti kitakuwa na matumizi mapana katika elimu na mafunzo, afya, viwanda, nishati, na utafiti.

Huu utakuwa mradi mkubwa zaidi wa Wakala wa Nishati na Nishati ya Nyuklia Kenya, ambao unahitaji dola milioni 246 kutekeleza mpango wake wa miaka mitano. Wakala huo unasema  tayari umepata ekari 65 za ardhi katika eneo la Konza Technopolis kwa ajili ya ujenzi wa kinu cha utafiti wa nyuklia na vifaa vingine vya kituo cha utafiti wa nyuklia.

Wakala wa Nishati na Nishati ya Nyuklia Kenya mnamo Septemba mwaka jana ulitangaza mpango wa kujenga kituo cha kuzalisha umeme nyuklia wa megawati 1,000 (MWe) katika kaunti za Kilifi au Kwale eneo la pwani.

Shirika hilo linasema ujenzi wa kinu hicho cha nyuklia utaajiri hadi wafanyikazi 7,000 katika kilele cha ujenzi na hadi wafanyikazi 700 wakati wa operesheni.