Jul 13, 2016 15:22 UTC
  • Riek Machar aondoka Juba, nchi za Ulaya zawaondoa raia wao Sudan Kusini

Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar ameondoka katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba pamoja na askari wanaomuunga mkono na kwenda kusikojulikana.

James Gatdet Dak, msemaji wa Machar ameliambia shirika la habari Reuters jijini Nairobi kuwa, Machar amelazimika kuondoka na vikosi vyake mjini Juba ili kuepusha mapigano zaidi katika nchi hiyo changa zaidi barani Afrika. Amesisitiza kuwa: "Machar hajarejea msituni, wala hapangi mapigano mapya bali ameondoka Juba kwa kuheshimu utekelezwaji wa makubaliano ya usitishaji vita ambayo yanaingia siku ya nne Alkhamisi hii."

Huku hayo yakiripotiwa, Ujerumani na Italia zimeanza kuondoa raia wao nchini Sudan Kusini kutokana na mapigano hayo.

Wakati huo huo serikali ya Juba imekosoa wito wa Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulitaka Baraza la Usalama la umoja huo kuiwekea Sudan Kusini vikwazo vya silaha. Balozi wa Sudan Kusini nchini Kenya, Chol Mawut Ajonga, amesema hajui lengo la vikwazo hivyo vya silaha na kuhoji kuwa: "Je wanataka wanajeshi wetu wabeba mabakora badala ya bunduki?"

Mapigano baina ya wafuasi wa Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na makamu wake Riek Machar mjini Juba, yamepelekea zaidi ya watu 300 kuuawa na maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao. Baadhi ya duru za habari zinasema idadi ya waliouawa katika mapigano hayo yaliyoanza Alkhamisi iliyopita yumkini imepindukia watu 1,000.

Tags