Hatima ya TV za Ikhwanul Muslimin nchini Uturuki haijulikani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11389-hatima_ya_tv_za_ikhwanul_muslimin_nchini_uturuki_haijulikani
Vyombo vya habari vya Misri vimetangaza kuwa, hatima ya televisheni za kundi la Ikhwanul Muslimin zilizokuwa zinarusha matangazo yake nchini Uturuki, haijulikani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 16, 2016 23:37 UTC
  • Hatima ya TV za Ikhwanul Muslimin nchini Uturuki haijulikani

Vyombo vya habari vya Misri vimetangaza kuwa, hatima ya televisheni za kundi la Ikhwanul Muslimin zilizokuwa zinarusha matangazo yake nchini Uturuki, haijulikani.

Mtandao wa habari wa al Yaumus Sabi'i umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, baadhi ya kanali hizo zimefungwa ghafla katika kipindi cha siku chache tu, bila ya kutolewa taarifa za kabla yake.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kanali hizo za Ikhwanul Muslimin zinazoongozwa na Ayman Nur, mkuu wa televisheni ya al Sharq na Mahmoud Hussein, Katibu Mkuu wa kundi la Ikhwanul Muslimn na mwasisi wa televisheni ya al Watan. Amesema, wakuu hao waandamizi wa Ikhwanul Muslimin wamenyamaza kimya na hawasemi chochote kuhusiana na kufungwa televisheni hizo.

Habari hiyo imekuja baada ya kushindwa jaribio la mapinduzi ya kijeshi la kumg'oa madarakani Rais Recep Tayyip Edrogan wa Uturuki la usiku wa kuamkia jana Jumamosi.

Miongoni mwa ugomvi uliopo baina ya Misri na Uturuki hivi sasa, ni Ankara kuwapa uhuru wafuasi wa Ikhwanul Muslimin kutangaza sera zao kwa uhuru nchini humo.

Kundi la Ikhwanul Muslimin hivi sasa lina kanali nne za televisheni nchini Uturuki zijulikanazo kwa majina ya al Sharq, al Watan, Mukammilin na al Hiwar. Televisheni hizo zinatuhumiwa kuchochea machafuko nchini Misri.