Watu milioni mbili wanakabiliwa na njaa nchini Madagascar
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1156-watu_milioni_mbili_wanakabiliwa_na_njaa_nchini_madagascar
Serikali ya Madagascar imetangaza kuwa, watu milioni mbili katika maeneo ya vijijini wanakabiliwa na njaa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu milioni moja wanakabiliwa na njaa katika eneo la kusini mwa nchi hiyo kufuatia ukame mkali uliyolikumba eneo hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 13, 2016 04:24 UTC
  • Watu milioni mbili wanakabiliwa na njaa nchini Madagascar

Serikali ya Madagascar imetangaza kuwa, watu milioni mbili katika maeneo ya vijijini wanakabiliwa na njaa. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu milioni moja wanakabiliwa na njaa katika eneo la kusini mwa nchi hiyo kufuatia ukame mkali uliyolikumba eneo hilo.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kufuatia kushadidi kwa ukosefu wa chakula, wakazi wa maeneo hayo wamelazimika kukusanya wadudu na kuwafanya chakula ili kuokoa maisha yao. Afisa mmoja wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO nchini Madagascar amenukuliwa akisema kuwa, hali ya sasa ya uhaba wa chakula katika eneo la kusini mwa nchi hiyo si mbaya tu, bali ni janga la kibinaadamu kwani ukosefu wa chakula unawakabili watu milioni mbili ndani ya taifa hilo. Mbali na wakazi wa maeneo ya kusini, wakazi wa maeneo mengine ya nchi hiyo ni miongoni mwa wahanga wa tatizo hilo. Madagascar ni nchi ya mwambao wa kusini mashariki mwa Afrika, ambayo mara kwa mara hukumbwa na matatizo ya uhaba wa chakula. Kabla ya hapo Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO lilikuwa limetangaza kuwa, taathira za mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na El Nino zitapelekea nchi nyingi Afrika ikiwemo Madagascar kukumbwa na ukame mkubwa na kwamba, mazao katika eneo hilo yatateketea kabisa. Nchi zingine ambazo raia wake wanakabiliwa na baa la njaa ni Malawi, Namibia, Ethiopia na Lesotho ambapo mamilioni ya watu wa nchi hizo wanakabiliwa na hatari ya kukumbwa na baa hilo la njaa.