Aug 25, 2024 14:59 UTC
  • Mali yasimamisha matangazo ya televisheni ya LCI ya Ufaransa kwa upotoshaji

Serikali ya kijeshi ya Mali imepiga marufuku kanali ya televisheni ya Ufaransa ya LCI kurusha matangazo yake kwa muda wa miezi miwili kutokana na kile kilichotajwa kuwa upotoshaji kuhusu hali ya usalama wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mamlaka ya Mawasiliano ya Mali (HAC) imesema katika taarifa kuwa: Huduma za televisheni ya LCI zimeondolewa kutoka kwa orodha ya wasambazaji wote wa huduma za utangazaji za redio au televisheni zilizoidhinishwa nchini Mali kwa muda wa miezi miwili kuanzia tarehe 23 Agosti.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya Kanali Michel Goya, afisa wa kijeshi kutoa maoni yaliyokosolewa na serikali ya Mali, katika kipindi cha LCI kilichorushwa hewani Julai 27 chini ya anuani ya "Wagner aliangamizwa nchini Mali: Mkono wa Kyiv." 

Mamlaka ya Mawasiliano ya Mali imesisistiza kuwa, "Wakati wa matangazo haya, ukiukwaji kadhaa wa vifungu vya sheria ulibainika."

Kanali Assimi Goita wa Mali (kushoto) na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Huko nyuma pia, serikali ya kijeshi ya Mali ilichukua hatua ya kusimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Ufaransa kwa muda wa miezi minne. Serikali ya kijeshi ya Mali wakati huo ilivituhumu vyombo hivyo vya habari kuwa vinaripoti habari za uwongo kwamba jeshi linaua raia.

Kadhalika serikali za Niger na Burkina Faso zimewahi kusimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.

Tags