Mashambulizi ya makombora ya wanamgambo wa RSF yaua takriban raia 21 katikati mwa Sudan
(last modified 2024-09-09T10:37:12+00:00 )
Sep 09, 2024 10:37 UTC
  • Mashambulizi ya makombora ya wanamgambo wa RSF yaua takriban raia 21 katikati mwa Sudan

Raia wasiopungua 21 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya wanamgambo wa kikosi cha radiamali ya haraka (RSF) kuvurumisha makombora sokoni katika mji wa Sinnar katikati mwa Sudan.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan umeripoti kuwa raia wasiopungua 21 wameuawa na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa katika mashambulizi ya makombora yaliyotekelezwa na kikosi cha RSF katika soko la Sinnar katikati mwa Sudan. Mtandao huo wa Madaktari wa Sudan umesema kuwa unalaani mauaji hayo ya umati yaliyofanywa na wanamgambo wa RSF dhidi ya raia katika mji wa Sinnar kwa kuyalenga maeneo ambayo watu hukusanyika na hivyo kusababisha maafa makubwa ya binadamu. 

Kikosi cha Radiamali ya Haraka kinachoongozwa na Mohamed Hamdan Daglo Makamu wa zamani wa mkuu wa baraza la uongozi la Sudan Juni 24 mwaka huu kilishambulia jimbo la Sinnar na kudhibiti miji kadhaa ya jimbo hilo. 

Mohamed Hamdan Daglo

Jeshi la Sudan (SAF) linapigana vita na Kikosi cha Radiamali ya Haraka (RSF) tangu katikati ya Aprili mwaka jana; ambapo hadi sasa watu zaidi ya elfu 20 wameuawa vitani na wengine karibu ya milioni 10 wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi katika nchi jirani. 

Jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa zinaendelea kupaza sauti zikitoa wito wa kusitishwa vita huko Sudan ili kuzuia maafa ya kibinadamu ambayo yatawasukuma mamilioni ya watu katika njaa na kifo kutokana na uhaba wa chakula uliosababishwa na mapigano ambayo tayari yameenea katika majimbo 13 kati ya 18 ya Sudan. 

 

Tags