Rais wa Guinea-Bissau: Mke wangu ameniasa nisigombee muhula wa pili
(last modified 2024-09-13T03:05:34+00:00 )
Sep 13, 2024 03:05 UTC
  • Rais wa Guinea-Bissau: Mke wangu ameniasa nisigombee muhula wa pili

Katika hatua ambayo imewashangaza wengi, Rais wa Guinea-Bissau Umaro Cissoko Embalo alisema jana Alkhamisi kwamba hatawania muhula wa pili katika uchaguzi wa rais unaotazamiwa kufanyika Novemba.

Wadadisi wa mambo wanasema tangazo hilo la ghafla linaweza kusababisha ombwe la uongozii na kuzidisha mivutano ya kisiasa katika nchi hiyo inayokabiliwa mara kwa mara na mapinduzi, yenye takriban watu milioni mbili.

Mwishoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri usiku wa kuamkia jana Alhamisi, Embalo alisema mke wake ndiye aliyemshawishi na kumtaka asigombee muhula wa pili wa urais.

Embalo alichaguliwa Januari 2020 kumrithi rais Jose Mario Vaz. Alimshinda hasimu wake Domingos Simoes Pereira aliyeibuka wa pili kwa 54% ya kura; na angeweza kugombea muhula mwingine kisheria. Rais Embalo mwenye umri wa miaka 51, hakumtaja mrithi wake.

Mwanasiasa Domingos Simoes Pereira aliyeibuka wa pili 2020

Ikumbukwe kuwa, Disemba mwaka jana, Embalo, alilivunja Bunge linalotawaliwa na upinzani, siku tatu baada ya mapigano ya silaha ambayo aliyataja kama "jaribio la mapinduzi" na ambayo yaliitumbukiza nchi hiyo ndogo ya Afrika Magharibi katika mgogoro mwingine.

Guinea-Bissau inasumbuliwa na misukosuko ya kisiasa na imekumbwa na msururu wa mapinduzi tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Ureno mwaka 1974; na mara ya mwisho ilikuwa Februari mwaka 2022.

Tags