Watu 55,600 wameathiriwa na mafuriko nchini Senegal
(last modified Sun, 20 Oct 2024 10:32:08 GMT )
Oct 20, 2024 10:32 UTC
  • Watu 55,600 wameathiriwa na mafuriko nchini Senegal

Serikali ya Senegal imetangaza kuwa, mafuriko katika Mto wa Senegal yameathiri familia 774 zenye karibu watu 55,600 za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mafuriko hayo yamekomba hekta 1,002 za mashamba na mazao makuuu ya nchi hiyo. Yamekomba asilimia 49.19 ya mashamba ya pilipili, asilimia 21.59 ya mashamba ya mpunga na silimia 10.56 ya mashamba ya mahindi ambayo yote yameharibiwa vibaya.

Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, ambaye amekuwa ziarani kulitembelea eneo la kusini-mashariki mwa nchi hiyo la Kedougou tangu Ijumaa ameendelea kufanya tathmini ya maeneo yaliyoathiriwa akiwa angani na ametembelea mji wa Bakel ili kuonyesha mshikamano wake na jamii zilizoathirika.

Rais huyo wa Senegal ametangaza kutenga faranga bilioni 8 takriban dola milioni 13.3 za Kimarekani kama juhudi za awali za kuuwasaidia waathirika wa mafuriko hayo. 

Kwa zaidi ya miaka ishirini, Senegal imekuwa ikikabiliwa na mafuriko makubwa katika kila msimu wa mvua kubwa unaoanzia mwishoni mwa mwezi Mei na kuendelea hadi Septemba.

Pape Goumba Lô, profesa katika Chuo Kikuu cha Dakar ambaye ni mwanajiolojia na mwanamazingira amesema kuwa, Senega ni peninsula inayokumbwa sana na mikondo ya maji kupita mipaka yake. Ni nchi yenye mabonde ambayo ni makazi ya vibanda na majengo ya kudumu ya kudumu ya watu.