Sudan na Sudan Kusini zajadili namna ya kuanzisha tena usafirishaji mafuta
(last modified Mon, 21 Oct 2024 02:47:33 GMT )
Oct 21, 2024 02:47 UTC
  • Sudan na Sudan Kusini zajadili namna ya kuanzisha tena usafirishaji mafuta

Sudan na Sudan Kusini jana Jumapili zilisisitizia haja ya kushughulikia vikwazo vinavyokwamisha juhudi za kuanzisha tena usafirishaji wa mafuta ya Sudan Kusini kupitia ardhi ya Sudan.

Haya yamekuja baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Mpito la Sudan ambaye pia ni Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan (SAF) Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan kukutana jana Jumapili na Mshauri wa Rais wa Sudan Kusini kuhusu Usalama wa Taifa, Tut Gatluak huko Port Sudan, makao makuu ya Jimbo la Bahari Nyekundu la mashariki mwa Sudan.

Katika taarifa yake, Gatuak amesema, Sudan Kusini iko tayari kutekeleza vipengee vya makubaliano baina yake na serikali ya Sudan. Aidha amesema: "Timu zote za kiufundi katika nchi hizi mbili ziko tayari kuongeza uzalishaji na kuhakikisha mafuta ya Sudan Kusini yanafika nje ya nchi kupitia bandari ya Bashayer ya Sudan.

Vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi vimekwamisha kila kitu nchini Sudan

 

Mwezi Machi mwaka huu, serikali ya Sudan ilitangaza kusimamisha mauzo ya mafuta ya Sudan Kusini kupitia maeneo ya Sudan kutokana na matatizo yaliyotokea katika njia za usafirishaji wa mafuta hayo.

Kwa mujibu wa serikali ya Sudan, tatizo hilo lilitokana na kuziba bomba la chini ya ardhi lililoko kaskazini mwa Jimbo la White Nile la Sudan, eneo ambalo linadhibitiwa na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinavyoshiriki kwenye vita vya uchu wa madaraka kati yake na Jeshi la Sudan (SAF).