Jul 25, 2016 08:08 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika machafuko mapya CAR

Kwa akali watu watatu wameuawa katika wimbi jipya la mashambulizi ya makundi ya waasi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Duru za polisi zimearifu kuwa, watu hao waliuawa katika makabiliano kati ya wafugaji na kundi la wabeba silaha katika mji wa Ngakobo, kusini mwa nchi. Habari zaidi zinasema kuwa, mamia ya watu wamelazimika kuukimbia mji huo kutokana na mapigano hayo yanayoaminika kuanzishwa na wafuasi wa zamani wa kundi la wapiganaji la Seleka.

Wakazi wa mji huo wanasema kufikia jana jioni, hali ya utulivu ilikuwa imerejea kwa kiasi fulani lakini makundi hayo ya wabeba silaha yangali yanazunguka zunguka katika vijiji vya mji huo.

Askari wa MONUSCO wakishikia doria

 

Haya yanajiri siku mbili baada ya taasisi za kiraia za Invisible Children na The Resolve kwa pamoja kutangaza kwamba, katika kipindi cha miezi sita ya mwaka huu wa 2016, jumla ya watu 344 wakiwemo watoto 65 wametekwa nyara na waasi wa Kikristo wa Anti-Balaka. Hii ni katika hali ambayo, nchi hiyo ina askari wapatao 12,000 wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa MUNUSCO.

Nchi hiyo ya katikati mwa Afrika ilitumbukia katika machafuko ya ndani mwaka 2013 baada ya makundi ya waasi kumfurusha aliyekuwa rais wa nchi hiyo François Bozizé.

Tags