Vyama vya upinzani Namibia vyapinga ushindi wa SWAPO katika uchaguzi wa rais
Dec 06, 2024 22:55 UTC
-
Bi Nandi-Ndaitwah
Kiongozi wa Chama cha Wazalendo Wanaojitegemea kwa ajili ya Mabadiliko (Independant Patriots for Change) nchini Nambia IPC Panduleni Itula amesisitiza kuwa hawayakubali matokeo ya uchaguzi wa rais yanayoonyesha mgombea wa chama tawala SWAPO ameshinda kwa zaidi ya 57% ya kura akiuita uchaguzi huo kuwa ni wa "fujo".
Panduleni Itula ameitaka mahakama ifute matokeo hayo na kuitisha uchaguzi mpya, huku akivishawishi pia vyama vya upinzani na wananchi kuungana pamoja kupinga kile alichokiita "ukandamizaji wa haki ya kupiga kura".
Ameashiria pia kukosekana karatasi za kupigia kura katika vituo mbalimbali na masuala kadhaa ya kiufundi yaliyojitokeza. Hali hiyo ilipelekea kurefushwa kwa muda wa siku tatu zoezi la upigaji kura katika baadhi ya maeneo ya nchi lililoanza Jumatano Novemba 27 na kuendelea hadi Jumamosi ya tarehe 30.
Kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Namibia ECN siku ya Jumanne, Bi Nandi-Ndaitwah alipata 57.31% ya kura, akimwacha nyuma mpinzani wake mkuu Panduleni Itula ambaye alipata 26%.
Upinzani una muda wa hadi wakati wa kabla ya kuapishwa Rais mteule mwezi Machi 21 2025 kuwasilisha hoja mahakamani za kuthibitisha kuwa uchaguzi wa rais haukutimiza vigezo na kuna ulazima wa kufanyika duru mpya ya uchaguzi.
Endapo ushindi wake hautabatilishwa na mahakama, Nandi-Ndaitwah atakuwa rais wa tano wa Namibia na kiongozi wa nne mwanamke barani Afrika kushika wadhifa huo baada ya Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia aliyeongoza nchi hiyo kati ya mwaka 2006 na 2018, Joyce Banda wa Malawi kutoka 2012 hadi 2014 na Samia Suluhu Hassan wa Tanzania aliyeko madarakani hivi sasa..../
Tags