Moto Madagascar wauwa watu 38, wakiwemo watoto 16
Watu zaidi ya 36 wamefariki dunia wakiwemo watoto 16 baada ya moto kutokea katika nyumba moja katikati mwa Madagascar.
Maafisa wa polisi wameeleza kuwa ajali hiyo ilitokea Jumamosi usiku wakati kulipokuwa kukifanyika hafla ya kusherehekea ukarabati wa nyumba katika wilaya ya Ikalamavony katikati mwa Madagascar. Watu waliohudhuria hafla hiyo ya kusherehekea kufanyiwa ukarabati nyumba ni pamoja na ndugu na jamaa wa mmiliki wa nyumba hiyo.
Msemaji wa polisi wa mkoa amesema kuwa watoto 16 ni miongoni mwa watu 38 walioaga dunia katika ajali hiyo ya moto.Ripoti zinasema kuwa wanavijiji walijaribu kuwanusuru watu katika moto huo hata hivyo walishindwa kufungua mlango wa nyumba. Kijana mwenye umri wa miaka 14 pekee ndiye aliyenusurika na moto huo baada ya kuruka dirishani. Moto huo unaaminika kusababishwa na mabua ya moto yaliyotumika mapema kupikia chakula cha wageni waalikwa. Madagascar ni kisiwa kilichoko katika bahari ya Hindi.