UN: Wakulima milioni 23 wanahitajia msaada kusini mwa Afrika
(last modified Fri, 29 Jul 2016 04:16:51 GMT )
Jul 29, 2016 04:16 UTC
  • UN: Wakulima milioni 23 wanahitajia msaada kusini mwa Afrika

Umoja wa Mataifa umesema wakulima milioni 23 katika nchi za kusini mwa Afrika wanahitajia msaada wa dharura kwa ajili ya kujiandaa na msimu ujao wa upaliliaji.

David Phiri, mshirikishi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO wa eneo la kusini mwa Afrika amesema wakulima hao wanahitajia mbegu, mbolea na suhula za kilimo kabla ya Oktoba, ili kuepusha mavuno ya mazao machache na hafifu katika msimu wa mavuno unaoanza Machi mwaka ujao 2017. Amesema asilimia 70 ya watu wa eneo hilo wanategemea kilimo kujikimu kimaisha na iwapo hawatapata msaada huo wa dharura, watalazimika kutegemea misaada ya kibinadamu hadi katikati ya mwaka 2018.

Athari za ukame barani Afrika

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, watu milioni 60, thuluthi mbili kati yao kutoka nchi za kusini na mashariki mwa Afrika wanakabiliwa na baa la njaa kutokana na ukame uliosababishwa na athari za el-Nino.

Mapema mwaka huu, Shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO lilitahadharisha kuwa, kutokana na kupungua sana mvua katika maeneo mengi ya kusini mwa Afrika na kutokuweko mazingira ya kupanda mazao katika akthari ya nchi za eneo hilo,  idadi kubwa ya watu watakosa chakula katika miezi ijayo. Kwa mujibu wa FAO, zaidi ya asilimia 42 ya wananchi wa Namibia wanakabailiwa na uhaba wa chakula. Kadhalika Malawi, Madagascar na Lesotho ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na uhaba wa chakula.