Magaidi 16 wa al-Shabaab wauawa katika operesheni ya jeshi la Somalia
(last modified Wed, 29 Jan 2025 10:37:29 GMT )
Jan 29, 2025 10:37 UTC
  • Magaidi 16 wa al-Shabaab wauawa katika operesheni ya jeshi la Somalia

Jeshi la Somalia limetangaza habari ya kuwaua magaidi 16 wa al-Shabaab katika operesheni katika mkoa wa Hiiraan, mashariki mwa nchi, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali.

Shirika la habari la Somalia SONNA limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, jeshi pamoja na vikosi vya ndani vimefanya operesheni kubwa katika eneo la Hiiraan kwa lengo la kulitokomeza kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda.

Taarifa hiyo imeleeza kuwa, vikosi vya usalama vya Somalia katika operesheni ya jana Jumanne vilitwaa kwa ufanisi maeneo kadhaa ya kimkakati, ikiwa ni pamoja na Beera Yabaal, Buur Abooto, Eega Galmaay, Jidcilaan, na Cadow Gureey.

Jeshi la serikali limesema operesheni yake inayoendelea inalenga kuikomboa kikamilifu Somalia kutoka kwa makundi yenye misimamo ya kufurutu ada, na kuhakikisha amani na usalama wa kudumu kwa raia wa Somalia.

Magaidi wa al-Shabab walioangamizwa

Nchi hiyo ya Pembe ya Afrika inakabiliwa na ukosefu wa usalama kwa miaka mingi sasa, huku genge la al-Shabaab na makundi ya kigaidi ya Daesh (ISIS) yakiwa tishio kuu kwa usalama wa nchi hiyo.

Tangu mwaka 2007, genge la kigaidi la al-Shabaab limekuwa likipigana na vikosi vya usalama vya serikali ya Somalia na askari walinda amani wa Umoja wa Afrika walioko nchini humo.