Watu 89 wauawa katika mashambulizi ya RSF Omdurman, Sudan
Raia wasiopungua 89 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwenye vijiji vya Omdurman, karibu na ufukwe wa Mto Nile, kaskazini magharibi mwa Khartoum, mji mkuu wa Sudan.
Chama cha Wanasheria wa Dharura kilisema katika taarifa kuwa, "Vikosi vya Msaada wa Haraka vimeshambulia zaidi ya vijiji 15 kusini mwa Omdurman tangu Machi 27."
"Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya watu 89 na mamia ya mamia kujeruhiwa kutokana na ufyatulianaji wa risasi, milio ya risasi ya moja kwa moja na mapigano ya silaha," taarifa ya chama hicho imeeleza.
Vijiji vilivyovamiwa na RSF ni "vya kiraia kabisa na havina vikosi vya kijeshi," ilisema taarifa hiyo, na kuongeza kuwa mashambulizi hayo ni "uhalifu kamili wa kivita unaolenga kuwatia hofu na kuwafukuza wakazi kwa nguvu."
Walioshuhudia tukio hilo waliambia Anadolu kuwa mamia ya wakaazi kutoka vijiji hivyo walikimbilia eneo la Jabal Awlia kutokana na mashambulizi hayo.

Haya yanajiri baada ya raia wengine 12 wa Sudan kuuawa katika mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) katika Jimbo la Kordofan Kusini.
Waasi wa RSF na mshirika wao Sudan People's Liberation Movement-North (SPLM-N) walitumia silaha nzito kushambulia maeneo ya makazi katika jimbo hilo la kusini mwa Sudan, ambapo makumi ya watu wamjeruhiwa pia.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumatano na kuongeza kwamba, mamia ya familia pia zimelazimika kukimbia makazi yao kutoka na mashambulio hayo katika eneo la Khor al-Dalib, yaliyoanza tangu Jumatatu.