KDF: Al-Shabaab inawasajili kwa nguvu vijana nchini Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12523-kdf_al_shabaab_inawasajili_kwa_nguvu_vijana_nchini_kenya
Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF limesema kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab sasa linawalazimisha vijana kujiunga nalo, haswa katika maeneo ya Pwani ya nchi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 03, 2016 08:01 UTC
  • KDF: Al-Shabaab inawasajili kwa nguvu vijana nchini Kenya

Jeshi la Ulinzi la Kenya KDF limesema kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab sasa linawalazimisha vijana kujiunga nalo, haswa katika maeneo ya Pwani ya nchi.

Kamanda Mkuu wa jeshi hilo Jenerali Samson Mwathethe amesema kundi hilo la kigaidi limepoteza ushawishi wa kuwarubuni vijana wajiunge nalo, na kwa msingi huo wameanza kuwasajili watu kwa nguvu.

Magaidi wa kundi la al-Shabaab

Jenerali Mwathethe amesema Kenya kama nchi nyingi duniani inakabiliwa na jinamizi la ugaidi na kusisitiza kuwa, ili kutokomeza harakati za kigaidi nchini, sharti kila mmoja awe macho na awe mwepesi wa kutoa taarifa na kuvipasha habari vyombo vya usalama juu ya harakati hizo katika maeneo yao.

Februari mwaka huu, watu wanne waliuawa kwa kufyatuliwa risasi na wanamgambo wa al-Shabaab katika kaunti ya Kwale, kwa kuliasi kundi hilo la kigaidi na kujisalimisha kwa vyombo vya dola.

Jeshi la Kenya hata hivyo linasisitiza kuwa litaendeleza operesheni zake za kijeshi dhidi ya wanachama wa kundi hilo ndani na nje ya nchi, ikiwemo operesheni iliyopewa jina la 'Linda Boni' kwa ajili ya kuondoa hatari tarajiwa ya kundi hilo la kitakfiri katika kaunti ya Lamu.