Viongozi wa Afrika wahudhuria hafla ya kuapishwa Rais Deby wa Chad
-
Rais Idris Deby wa Chad
Rais Idris Deby wa Chad anatazamiwa kula kiapo cha kulitumikia taifa hilo kwa muhula wa tano, baada ya kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Miongoni mwa marais na viongozi wa Afrika wanaotazamiwa kuhudhuria hafla ya kuapishwa Rais Deby katika mji mkuu N’Djamena ni Rais Patrice Talon wa Benin, Rock Mark Kabore wa Burkina Faso, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda, Rais wa Equatorial Guinea Theodoro Obiang Nguema Mbasogo miongoni mwa wengine.
Itakumbukwa kuwa, Aprili 22, Tume ya Uchaguzi nchini Chad ilimtangaza Rais Déby kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 60 ya kura, huku mpinzani wake, Saleh Kebzabo akipata asilimia 12 ya kura hizo.
Licha ya timu ya waangalizi wa Umoja wa Afrika kusema kuwa uchaguzi nchini Chad ulifanyika katika anga huru na salama, lakini Kebzebo alipinga matokeo hayo akisema kuwa, kulifanyika uchakachuaji mkubwa wa kura kwa maslahi ya Rais Déby.
Rais Déby amekuwa madarakani tangu mwaka 1990, baada ya kumuondoa madarakani aliyekuwa rais wa nchi hiyo, dikteta Hissène Habré.