Taasisi ya misaada Sudan: Shambulio la RSF limeua watu 75 Darfur
Vikosi vya Usaidizi wa Haraka RSF vimewaua watu 75 katika shambulio la ndege zisizo na rubani lililolenga msikiti mmoja katika kambi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao kwenye jimbo la Darfur nchini Sudan. Hayo yameelezwa na taasisi ya utoaji misaada inayoendesha eneo hilo inayojulikana kama Chumba cha Mjibizo wa Dharura (Emergency Response Room).
Shambulio hilo lilifanywa jana Ijumaa wakati wanamgambo wa RSF walipokuwa wakijaribu kulirejesha nyuma jeshi katika mji wa Al Fasher, makao makuu ya jimbo la Darfur.
Taarifa iliyotolewa na taasisi hiyo ya misaada imesema: "miili imetolewa kutoka kwenye vifusi vya msikiti".
Kwa upande mwingine, picha za satalaiti zimeonyesha kuwa RSF inasonga mbele katika mji huo wa Al Fasher uliowekewa mzingiro.
Kwa muda wa karibu miezi 18, Al Fasher imewekewa mzingiro na wanamgambo wa vikosi vya usaidizi wa haraka ambavyo tayari vinadhibiti sehemu za makao makuu ya jimbo la Darfur Kaskazini.
Jeshi la Sudan, SAF ambalo ngome zake huko Al Fasher zimejikita zaidi upande wa magharibi, limekuwa katika vita na mapigano makali na vikosi vya RSF tangu Aprili 2023.../