Aug 12, 2016 15:03 UTC
  • Maandamano ya kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru yaendelea Nigeria

Kwa mara nyingine Waislamu nchini Nigeria wamefanya maandamano ya amani wakitaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky, kiongozi wa harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Mamia ya Waislamu wamemiminika mabarabarani katika jimbo ka Kano, kaskazini mwa nchi hiyo na kutaka kuachiliwa huru haraka iwezekanavyo kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu nchini Nigeria. Hii ni katika hali ambayo maelfu ya wananchi mjini Abuja, mji mkuu wa Nigeria walifanya maandamano makubwa hapo siku ya Jumatano katika kulalamikia hatua ya serikali ya Rais Muhammadu Buhari ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu wa taifa hilo na kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim El Zakzaky anayeendelea kuwekwa kizuizini.

Waislamu Nigeria wakitaka kuachiliwa Sheikh Zakzaky

Ni miezi minane sasa imepita tangu kiongozi huyo wa Kiislamu na mke wake Zeenat walipotiwa mbaroni na jeshi la Nigeria. Hii ni katika hali ambayo hali ya kiafya ya kiongozi huyo imetajwa kuwa mbaya mno, hata hivyo viongozi wa nchi hiyo hawako tayari kusikiliza malalamiko ya wananchi ya kumuachilia huru.

Waislamu Nigeria

Katika uvamizi wa jeshi la Nigeria kwenye makazi ya Sheikh huyo mjini Zariya katika jimbo la Kaduna kaskazini mwa nchi hiyo na pia dhidi ya Husseiniyyah ya Waislamu wa Kishia hapo tarehe 14 Disemba mwaka jana 2015, karibu Waislamu 1000 waliuawa. Kadhalika jeshi hilo lilimjeruhi kwa risasi kadhaa Sheikh Ibrahim Yaqoub El Zakzaky na mke wake na kisha kuwatia mbaroni na kuendelea kuwashikilia hadi sasa.

Tags