Korea Kusini yadai: Askari wa Korea Kaskazini wanapigana bega kwa bega na Russia Ukraine
Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini amesema, inavyoonekana wanajeshi wa Korea Kaskazini wanapigana bega kwa bega na wanajeshi wa Russia nchini Ukraine.
Madai hayo yanatolewa huku Pyongyang na Moscow zikiimarisha zaidi uhusiano wao wa pande mbili. Korea Kaskazini ilishakanusha hapo kabla tuhuma kwamba inavipatia silaha vikosi vya Russia katika mapigano kati yake na vikosi vya Ukraine.
Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini ameendelea kusema: "kwa kuzingatia hali kadhaa, tunatathmini taarifa za uwezekano mkubwa wa kuwepo majeruhi miongoni mwa maafisa na wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Ukraine" na akaongeza kuwa, Seoul inatarajia Pyongyang itatuma wanajeshi zaidi kuisaidia Russia katika vita baina yake na Ukraine.
Mnamo mwezi Juni, Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un na Rais Vladimir Putin wa Russia waliidhinisha ushirikiano wa kimkakati wa kina ambao unajumuisha makubaliano ya ulinzi wa pande zote kati ya nchi hizo mbili.
Korea Kusini, ikiungwa mkono na Marekani, inadai kuwa Pyongyang imekuwa muuzaji mkuu wa silaha zinazotumiwa na Russia nchini Ukraine. Hata hivyo Pyongyang na Moscow zimekanusha madai hayo.../