Tume: Uchaguzi nchini CAR umefanyika kwa amani
Uchaguzi Mkuu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati umefanyika katika mazingira ya utulivu na amani.
Mtandao wa habari wa All African umemnukuu Marie Madeleine NKouet Hoornaert, mkuu wa tume ya taifa ya uchaguzi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati akisema hayo na kuongeza kuwa, pamoja na kuwepo matatizo ya hapa na pale katika mchakato wa uchaguzi wa Rais na Bunge wa jana Jumapili, lakini kiujumla ni kuwa uchaguzi huo umefanyika katika mazungira mazuri na ya amani.
Hata hivyo kumeripotiwa pia kesi kadhaa za kuweko mpangilio mbovu bali hata kumeripoti wapiga kura kupigana katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Duru ya pili ya uchaguzi wa rais na duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge la Jamhuri ya Afrika ya Kati zilifanyika jana baada ya kuripotiwa kesi nyingi wakati wa kupiga kura katika uchaguzi wa awali na kupelekea kuakhirishwa uchaguzi huo hadi jana.
Wagombea wawili Anicet Georges Dologuélé na Faustin Touadéra ndio waliochuana kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa Rais.
Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanatumai kuwa, kufanyika kwa usalama na amani uchaguzi huo kutamaliza miaka mitatu ya machafuko nchini mwao.