Aug 22, 2016 03:56 UTC
  • Mgogoro wa kiuchumi wa Nigeria

Nigeria imeikabidhi Afrika Kusini nafasi yake kama nchi ya kwanza yenye uchumi wenye nguvu kuwba zaidi barani Afrika.

Gazeti la Kifaransa la Le Point limeandika kuwa, Nigeria ambayo kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita imekuwa na ustawi mkubwa wa kiuchumi na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika, inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kiuchumi kiasi kwamba imeshindwa kulipa hata madeni yake. Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni za uchumi, Afrika Kusini ilichukua nafasi ya Nigeria kama nguvu kubwa zaidi ya kiuchumi barani Afrika tangu mwaka 2014. 

Kwa sasa uchumi wa Nigeria uko katika hali mbaya kiasi kwamba, baadhi ya duru zinaripoti kuwa uchumi wa nchi hiyo umekumwba na mdororo. Katika fremu hiyo, thamani ya safaru ya Nigeria, Naira, imeporomoka sana wiki hii na kufikia kiwango cha chini. Wakati huo huo migogoro ya kisiasa na machafuko navyo vimeendelea kushuhudiwa nchini Nigeria. Harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram nchini humo na nchi nyingine jirani zimesababisha sehemu kubwa ya pato la serikali litumiwe katika kupambana na genge hilo.

Rais Buhari ana wasiwasi mkubwa kutokana na harakati za makundi ya Niger Delta, Boko Haram

Kwa sasa moja ya malengo muhimu ya Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria na viongozi wa nchi jirani, ni kuzidisha mapambano kwa lengo la kuliangamiza kabisa kundi hilo katika eneo. Kwa sababu hiyo wakati, bajeti na nguvu kubwa ya nchi hiyo vinaelekezwa katika sekta hiyo.

Katika upande mwingine, asilimia 70 ya pato la serikali ya Nigeria inadhaminiwa na mauzo ya mafuta ya petroli. Kwa hakika Nigeria ni sawa na nchi nyingine wazalishaji wa mafuta ambazo zimeathirika pakubwa kutokana na kupungua kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia. Kupungua kwa pato litokanalo na mafuta ya petroli kumeifanya serikali ya Abuja ikumbwe na nakisi kubwa ya bajeti na hivyo kuzidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Tarehe 11 mwezi huu Rais Muhammadu Buhari alihutubia taifa akisema kuwa, Nigeria imegeuka na kuwa nchi masikini. Sambamba na suala hilo, mashambulizi yanayofanywa na kundi la waasi wa Niger Delta dhidi ya taasisi za mafuta huko kusini mwa nchi hiyo yameathiri pia kiwango cha uzalishaji wa bidhaa hiyo. Kundi la waasi wa Niger Delta linaamini kuwa mashirika ya kigeni yanapora utajiri wa taifa na hivyo linataka yaondoke nchini Nigeria. Kadhalika kundi hilo linataka kutengwa sehemu kubwa ya pato la mafuta kwa ajili ya eneo hilo.

Mambo hayo na mengine ndio yaliyoitumbukiza Nigeria katika hali mbaya ya kiuchumi kiasi kwamba, wiki iliyopita Bettina Luescher, Msemaji wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO ) alitangaza kuwa mgogoro wa chakula unaotokana na mashambulizi ya miaka kadhaa ya wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram umesababisha zaidi ya watu milioni tatu wakazi wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wakumbwe na uhaba mkubwa wa chakula. Luescher akiwa mjini Geneva alisema kuwa, hali ngumu ya uchumi ya Nigeria iliyosababishwa na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na kadhalika mfumuko wa bei unaotarajiwa kupanda zaidi mwezi ujao, ni mambo ambayo yanatazamiwa kuongeza idadi ya waathirika wa janga la njaa na kufikia milioni tano.

Bettina Luescher, Msemaji wa FAO

Licha ya kwamba weledi wengi wa masuala ya uchumi wanatabiri kuwa kuna matumaini  ya kupatikana maendeleo ya kisiasa na fursa za kuvutia wawekezaji wa kigeni katika nchi za Kiafrika, lakini kuongezeka kwa makundi ya kigaidi, vita vya ndani na machafuko katika nchi kadhaa za Afrika vimekwamisha ustawi wa uchumi wa nchi nyingi. Hivi sasa sio Nigeria pekee, bali nchi nyingi za Kiafrika zinakabiliwa na changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Inaonekana mazingira hayo ndio yamezifanya nchi za Kiafrika kuimarisha ushirikiano wao katika sekta tofauti za kiuchumi, kiusalama na kisiasa. Kuongezeka mabadilishano ya kiuchumi na kuondoa vizuizi, kuimarisha usalama wa ndani na kadhalika kuimarisha demokrasia, umoja na juhudi kwa ajili ya kupambana kwa pamoja na makundi ya kigaidi kama Boko Haram na ash-Shabab ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na nchi hiyo.

Tags