Ufaransa yaitaka serikali ya Libya izungumze na makundi ya nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14554-ufaransa_yaitaka_serikali_ya_libya_izungumze_na_makundi_ya_nchi_hiyo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameyataka makundi ya Libya yatatue matatizo yao na serikali ya umoja wa kitaifa na yaisaidie serikali hiyo katika jitihada zake za kuleta umoja na kupambana na mifarakano nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 03, 2016 11:45 UTC
  • Jean-Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa
    Jean-Marc Ayrault, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameyataka makundi ya Libya yatatue matatizo yao na serikali ya umoja wa kitaifa na yaisaidie serikali hiyo katika jitihada zake za kuleta umoja na kupambana na mifarakano nchini humo.

Jean-Marc Ayrault alitoa mwito huo jana mbele ya mabalozi wa Ufaransa mjini Paris na kusema kuwa, makundi ya Libya kama vile Bunge la Tobruk na kundi la Jenerali Khalifa Haftar ambaye ni mkuu wa vikosi vya ulinzi mashariki mwa Libya yanapaswa kuitambua rasmi serikali ya umoja wa kitaifa ya Waziri Mkuu Fayez al Sarraj.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa ameongeza kwamba, ijapokuwa kuna wasiwasi kuhusu masuala mbalimbali, na serikali ya umoja wa kitaifa inaendesha mapambano makali ya kuliangamiza kundi la kigaidi la Daesh ili baadaye iweze kudhibiti maeneo yote ya Libya, lakini serikali hiyo inapaswa kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Bunge la Tobruk na kundi la Jenerali Khalifa Haftar ambaye ndiye anayeongeza vikosi vya ulinzi mashariki mwa Libya.

Waziri Mkuu wa Libya, Fayez al Sarraj

 

Wanajeshi wa Ufaransa wametumwa mashariki mwa Libya na hivi karibuni Paris ililazimika kukiri kuwa wanajeshi wake watatu waliuawa katikati ya mwezi Julai nchini humo na pia kukiri kuwa wanajeshi wake wanafanya kazi ya kukusanya taarifa za kijasusi kwa ajili ya vikosi vya ulinzi vilivyoko chini ya Khalifa Haftar.

Mwito wa Ufaransa wa kutaka serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya ikae kwenye meza ya mazungumzo na makundi hayo ya Libya umetolewa baada ya serikali hiyo kushindwa kupata imani ya bunge la Libya katika kikao cha siku ya Jumatatu cha bunge hilo. Wabunge wa Libya wametaka kuundwa upya serikali ya umoja wa kitaifa, au kuundwe serikali ndogo tu isiyo na mamlaka ya kila kitu.