Viongozi wa Waislamu Kenya walaani wanawake magaidi waliokuwa wamevaa buibui
Viongozi wa Waislamu nchini Kenya wamewakana na kuwalaani wanawake watatu waliotekeleza hujuma ya kigaidi dhidi ya kituo cha polisi mjini Mombasa siku ya Jumapili.
Wakizungumza Jumatatu, wamesema wameshtushwa na hatua ya wanawake kutekeleza hujuma ya kigaidi wakiwa wamevalia mavazi ya Kiislamu ya Hijabu aina ya Buibui. Aidha wamebainisha wasiwasi wao kuhusu kuongezeka wanawake Waislamu ambao wanajiunga na makundi wa kigaidi huku wakiwa tayari kuenda kupigana mstari wa mbele.
Akizungumza wakati wa sherehe za Idul Adha mjini Mombasa, Kadhi Mkuu wa Kenya Sharif Muhdhar amelaani vikali hujuma hiyo ya Jumapili na kusema Uislamu ni dini ya amani na kwamba wale wanaotekeleza hujuma za kigaidi wakiwa wamevalia mavazi ya Kiislamu wanaichafulia jina dini hii tukufu. Amesema wakati umefika sasa wa kuchukuliwa hatua kali dhidi ya kila ambaye anajihusisha na vitendo vya kigaidi bila kujali jinsia au dini yake.
Kwa upande wake, Senata Hassan Omar wa Mombasa amesema shambulio hilo linapaswa kuchukuliwa kwa uzito kwani ndio mara ya kwanza wanawake wanatumika moja kwa moja kutekeleza hujuma ya kigaidi. Aidha ametoa wito kwa Waislamu kushirikiana na maafisa wa usalama ili kukabiliana na tatizo la kigaidi.
Siku ya Jumapili asubuhi wanawake watatu waliokuwa wamevalia Hijabu waliingia katika kituo cha polisi cha central mjini Mombasa na kutekeleza hujuma ambapo waliwajeruhi maafisa wa polisi. Wanawake hao waliojitangaza kuwa wafuasi wa kundi la kigaidi la Al Shabab waliuawa katika hujuma hiyo.