UN: Wakimbizi 70,000 wa Dadaab wanataka kurudu Somalia
Umoja wa Mataifa umesema robo ya wakimbizi wa Kisomali wanaoishi katika kambi ya Dadaab nchini Kenya wametangaza utayarifu wao wa kurejea nchini kwao Somalia karibuni hivi.
Duke Mwancha, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR amesema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika hilo kati ya mwezi Julai na Agosti mwaka huu, wakimbizi 70,000 kati ya 284,000 wa Kisomali walioko katika kambi ya Dadaab, kaskazini mashariki mwa Kenya wamesema wako tayari kurejea nchini kwao hivi karibuni. Hata hivyo msemaji huyo wa UNHCR amesisitiza kuwa, hiyo haimaanishi kwamba wakimbizi 214,000 waliosalia hawana nia na azma ya kurejea nchini kwao.
Hivi karibuni Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR lilisema kuanzia mwezi Disemba mwaka 2014 hadi sasa, wakimbizi zaidi ya 30,000 wa Somalia wamerejeshwa kwa hiari katika nchi yao kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab.
Miezi kadhaa iliyopita serikali ya Kenya ilitangaza mpango wa kuifunga kambi ya Dadaab kikamilifu kufikia mwezi Mei mwaka 2017 kutokana na sababu za kiusalama, kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo uamuzi huo na Kenya umekabiliwa na upinzani mkubwa huku viongozi mbalimbali wa nchi za eneo hilo na taasisi za kimataifa wakisisitiza kuwa uamuzi huo wa Kenya wa kuifunga kambi ya wakimbizi ya Dadaab ni kinyume na sheria za kimataifa zinazowalinda wakimbizi.