Oct 06, 2016 14:23 UTC
  • 11 wauawa,  14 watoweka katika mapigano Jamhuri ya Afrika ya Kati

Habari kutoka Bangui, mji mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati zinaarifu kuwa, watu zaidi ya 11 wameuawa huku wengine 14 wakitoweka kufuatia mapigano makali yaliyojiri baada ya kuuawa mwanajeshi wa nchi hiyo ya kati kati mwa Afrika.

Herve Verhoosel, msemaji wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo amethibitisha habari za kuuawa watu 11 na kuongeza kuwa, 14 hawajulikani waliko huku wengine 14 wakijeruhiwa katika mapigano hayo yaliyojiri wiki hii katika eneo la PK5, viungani mwa mji mkuu Bangui, baada ya kuuawa Marcel Mombeka, kamanda wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo.

Wanajeshi wa Kulinda wa Amani wa Umoja wa Mataifa huko CAR

Mombeka ambaye pia aliwahi kuwa mpambe wa rais wa zamani Catherine Samba-Panza, aliuawa kwa kufyatuliwa risasi akiwa kwenye gari lake Jumanne iliyopita.

Haya yanajiri siku chache baada ya mashirika kadhaa ya kutoa misaada ya kibinadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kusimamisha shughuli zao katika nchi hiyo kwa kile yalichokieleza kuwa, ni kushambuliwa wafanyakazi wao.

Waasi wa Anti-Balaka wamekuwa wakitekeleza jinai za kutisha CAR

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Septemba, katika hotuba yake kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, Rais Faustin-Archange Touadéra wa Jamhuri ya Afrika ya Kati alisema kuwa, serikali yake imetekeleza hatua za kiusalama na kijamii na kuahidi kufanya juhudi kubwa kwa ajili ya kupambana na uhalifu na ufisadi wa kifedha. 

Tags