Mazungumzo ya Marais wa Misri na Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16903-mazungumzo_ya_marais_wa_misri_na_sudan
Misri na Sudan ni nchi mbili jirani zenye mivutano katika masuala mbalimbali. Mivutano hiyo imewafanya viongozi wa nchi hizo kukutana na kutiliana saini hati ya ushirikiano wa kiistratijia kama juhudi za kupunguza mivutano hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 07, 2016 02:30 UTC
  • Mazungumzo ya Marais wa Misri na Sudan

Misri na Sudan ni nchi mbili jirani zenye mivutano katika masuala mbalimbali. Mivutano hiyo imewafanya viongozi wa nchi hizo kukutana na kutiliana saini hati ya ushirikiano wa kiistratijia kama juhudi za kupunguza mivutano hiyo.

Marais Abdul Fattah el Sisi na Omar al Bashir wa Misri na Sudan walikutana jana mjini Cairo Misri na kutiliana saini hati hiyo ya ushirikiano wa kiistratijia pamoja na makublaiano 17 ya ushirikiano katika nyuga tofauti.

Misri na Sudan ni wanachama wa Umoja wa Afrika. Misri ni katika wanachama muhimu na ndiyo nchi kubwa zaidi ya Kiarabu katika umoja huo. Sudan kwa upande wake ndiyo nchi kubwa zaidi ya Kiarabu katika upande wa ukubwa wa ardhi yake, lakini mwaka 2011 Sudan ilimeguka kwa kujitenga Sudan Kusini. Katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano wa Misri na Sudan umeshuhudia mivutano na mizozo mingi. Mizozo mikubwa baina ya nchi hizo mbili ni ya kijiografia, maji na kisiasa. Upande wa kijiografia ni kwamba Sudan na Misri zina mizozo ya muda mrefu ya mipaka. Nchi hizo mbili zina mgogoro wa muda mrefu kuhusiana na umiliki wa maeneo ya  Hala'ib, Shalateen, Abu Ramad. Maeneo hayo yalidhibitiwa na Misri mwaka 1995 wakati Sudan inasema kuwa, maeneo hayo ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya Sudan. 

Maeneo yenye mzozo katika mpaka wa Misri na Sudan

 

Katika upande wa mizozo ya maji pia, nchi hizo mbili zina mizozo na hitilafu nyingi. Mto wa Nile ambao ndio mshipa wa uhai kwa Misri na mto mrefu zaidi duniani, unapitia nchini Sudan kabla ya kuingia Misri na kuwaga maji yake katika bahari ya Mediterranean. Mto huo unapita katika nchi 10 za Afrika zikiwemo Misri na Sudan na nchi zote hizo zinanufaika sana na maji ya mto huo. Hivi sasa serikali ya Ethiopia inafanya juhudi za kufaidika zaidi na maji ya mto huo, na imeamua kujenga bwawa la al Nahdha. Hata hivyo ujenzi wa bwawa hilo umekumbwa na hasira kali za Misri, wakati serikali ya Sudan inaunga mkono mradi huo wa Ethiopia. 

Uungaji mkono huo wa Sudan kwa mpango Ethiopia umekuwa sababu ya kuharibika uhusiano wa Misri na Sudan. Ni kwa sababu hiyo ndio maana suala hilo likawa moja ya ajenda za mazungumzo ya Rais Omar al Bashir wa Sudan na Rais Abdul Fattah el Sisi wa Misri, mjini Cairo. Maafisa wa wizara za mambo ya nje za nchi hizo mbili nao walionana mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana pambizoni mwa kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kujadiliana suala la bwana la al Nahdha la nchini Ethiopia.

Ujenzi wa bwawa la al Nahdha nchini Ethiopia

 

Mgogoro mwingine mkubwa baina ya nchi mbili za Misri na Sudan ni kila upande kuwa mwenyeji wa wapinzani wa serikali za upande wa pili. Sudan ni mwenyeji wa baadhi wa wafuasi wa Ikhwanul Muslimin, kundi ambalo serikali ya Misri inadai ni la kigaidi. Malalamiko hayo ya Misri yanatolewa pia kwa nchi za Uturuki na Qatar kutokana na kuweko huko wanachama wa Ikhwanul Muslimin. Sudan nayo inailalamikia Misri kwa kuwa mwenyeji wa baadhi ya viongozi wanaoipinga serikali ya Khartoum. 

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, kutiwa saini hati hiyo ya ushirikiano wa kiistratijia na makubaliano 17 ya ushirikiano baina ya nchi hizo mbili kunaweza kusaidia kutatua mizozo yote hiyo. Mtazamo huo wa weledi wa mambo unatiliwa nguvu na msimamo wa serikali ya Misri ambayo hivi sasa imeelekeza juhudi zake katika kutatua hitilafu zilizopo baina yake na majirani zake hususan nchi za Afrika.