Libya yatahadharishwa kuhusu mashambulizi zaidi ya Daesh
Mkuu wa Shirika la Mafuta la Taifa nchini Libya ametahadharisha kwamba, kuna uwezekano kundi la kigaidi la Daesh likafanya mashambulizi zaidi dhidi ya taasisi na vituo vya mafuta nchini humo maadamu hakujaundwa serikali ya umoja wa kitaifa.
Mustafa Sin'ullah amesema, Alkhamisi na Ijumaa iliyopita wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh walishambulia taasisi za mafuta za Libya na kuchoma moto medani ya mafuta ya al Fada na kusababisha hasara kubwa. Medani ya visima vya mafuta ya al Fada iko kusini magharibi mwa visima vya mafuta vya Al Sadr na Ras Unuf ambavyo vimekuwa vikishambuliwa mara kwa mara na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Daesh.
Libya ilitumbukia katika ghasia na machafuko ya ndani baada ya kuondolewa madarakani utawala wa kidikteta wa Muammar Gaddaf. Baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kwa sasa yanadhibitiwa na kundi la kigaidi la Daesh.