Machafuko yashtadi Jamhuri ya Afrika ya Kati
Hali ya usalama nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati imeripoti kuwa ya kutisha.
Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, hali ya usalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ni ya kuogofya kutokana na kuongezeka ghasia za utumiaji silaha. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, njia pekee inayoweza kuisadia Jamhuri ya Afrika ya Kati kuepukana na mgogoro ilio nao ni kuanza mazungumzo na makundi yote.
Wakati huo huo, ujumbe wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) leo umeeleza kuwa, mapigano makali yaliyojiri siku mbili zilizopita kati ya wanajeshi wa kikosi hicho na watu wenye silaha katika mji wa Bambari mkoani Ouaga ulioko umbali wa kilomita 250 kutoka mji mkuu Bangui yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 25 .
Hii ni katika hali ambayo ukosoaji dhidi ya wanajeshi hao wa MINUSCA wapatao elfu 13 umeendelea kuongezeka katika wiki mbili za hivi karibuni kutokana na wananchi kutoridhishwa na utendaji wa vikosi hivyo katika kuwalinda raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Wakat huo huo makundi ya kiraia ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yametoa wito wa kufanyika mgomo wa nchi nzima yakitaka askari wa MINUSCA waondoke nchini humo. Kikosi cha MINUSCA kimesema kuwa kitawachukulia hatua wale wote wanaotaka kuvuruga juhudi za mamlaka zilizochaguliwa kidemokrasia kwa lengo la kurejesha amani na uthabiti huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.