Jeshi la Kenya laua magaidi 140 wa Al Shabab nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i18544-jeshi_la_kenya_laua_magaidi_140_wa_al_shabab_nchini_somalia
Jeshi la Ulinzi la Kenya, KDF, limetangaza kuwaua magaidi 140 wa kundi la kitakfiri la Al Shabab katika jimbo la Lower Jubba, mjini Afamadow nchini Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 31, 2016 23:13 UTC
  • Jeshi la Kenya laua magaidi 140 wa Al Shabab nchini Somalia

Jeshi la Ulinzi la Kenya, KDF, limetangaza kuwaua magaidi 140 wa kundi la kitakfiri la Al Shabab katika jimbo la Lower Jubba, mjini Afamadow nchini Somalia.

Taarifa zinasema katika mapigano  yaliyochukua masaa matatu, magaidi 500 wa Al Shabab wakiwa na magari manane yenye mizinga pamoja na malori manne walijaribu kuuteka mji huo kwa kushambulia vituo vya jeshi la Somalia. Magaidi hao awali walishambulia kituo cha polisi kabla ya kurudishwa nyuma na wanajeshi wa eneo la Jubaland na Jeshi la Kitaifa la Somalia kabla ya kikosi maalumu cha KDF kuwasili na kuwafurusha.

Taarifa zinasema kikosi cha makomando wachache wa kikosi maalumu cha KDF kiliwazingira magaidi hao na kuua 140 miongoni mwao kabla ya kuteketeza magari kadhaa waliyokuwa wakitumia.

Magaidi wa al Shabab

Wakati huo huo magaidi 8 wa kundi la Al-Shabaab na wanajeshi wanne wa jeshi la serikali ya Somalia waliuawa siku ya Jumamosi kwenye mapambano makali yaliyotokea karibu na mji wa Baidoa, kusini magharibi mwa Somalia. Waziri wa habari wa jimbo la kusini magharibi mwa Somalia Bw. Ugaas Hassan, amesema kundi la Al-Shabaab lilishambulia kituo cha jeshi baada ya askari wa jeshi la serikali kuwaua wenzao.

Ni karibu miaka 25 sasa ambapo Somalia haina serikali kuu tangu alipopinduliwa dikteta Muhammed Siad Barre mwaka 1991. Tangu wakati huo machafuko yameikumba nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ambapo yameziathiri pia nchi jirani ikiwemo Kenya.