Nov 02, 2016 14:30 UTC
  • 38 wauawa na kujeruhiwa katika mapigano Niger

Watu 18 wameuawa na wengine zaidi ya 20 wamejeruhiwa katika mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji nchini Niger.

Habari zinasema kuwa, mapigano hayo ya jana yalitokea katika kijiji kimoja mjini Bangui, kusini mwa nchi karibu na mpaka na Nigeria baada ya mifugo ya wafugaji wa kabila la Fulani kuvamia mashamba ya wakulima wa eneo hilo.

Oumarou Mohamane, Meya wa mji wa Bangui amethibitisha kutokea mapigano hayo na kusema kuwa, polisi walilazimika kuingilia kati na kuzima mapigano hayo ya wakulima na wafugaji, ambapo mbali na mauaji na majeraha, nyumba zaidi ya 15 ziliteketezwa moto.

Waasi wanaobeba silaha nchini Niger

Mapigano kati ya wakulima na wafugaji wa kuhamahama yamekuwa yakishuhudiwa kila uchao katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, kutokana na uhaba wa maji na rasilimali mbali na mizozo ya ardhi.

Mbali na mapigano kati ya wafugaji na wakulima na harakati za uasi nchini Niger, nchi hiyo ya Kiafrika vile vile imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi kama Boko Haram yenye makao yake makuu katika nchi jirani ya Nigeria.

Mapema mwezi uliopita wa Mei, Wizara ya Ulinzi ya Niger ilisema kuwa wanajeshi wake 22 wameuawa na watu wenye silaha na kwamba kundi lililofanya shambulizi hilo limekimbilia upande wa Mali. Haikubainika iwapo lilikuwa kundi la kigaidi au la waasi.

Tags