Hizbullah yasisitizia uhusiano mwema na harakati ya Hamas
Mjumbe wa mrengo wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon, Hassan Hubullah, amesisitiza udharura wa kuimarishwa uhusiano mwema baina ya harakati hiyo na ile ya Palestina Hamas katika ngazi ya viongozi.
Hubullah ameyasema hayo kupitia mahojiano na Shirika la Habari la Quds Press na kuongeza kuwa, mbali na njia kadhaa za mawasiliano baina ya harakati hizo, pande mbili zina uhusiano imara na wa kihistoria na kwamba uhusiano huo kamwe hautakatika.
Mjumbe wa mrengo wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon, amesisitiza kuwa lengo la pamoja kati ya harakati hizo ni kupambana na utawala vamizi wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa, Hizbullah na Hamas kwa pamoja zinapinga vikali ugaidi na makundi yenye misimamo ya kufurutu ada ingawa kila upande una maoni yake maalumu kuhusiana na kadhia ya Syria. Hubullah ameweka wazi kwamba, Hamas haina mitazamo inayopingana sana na Hizbullah na kwamba harakati hiyo ya Palestina haijawahi kutangaza uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi ya Daesh na Jab'hatu Nusra.
Matamshi ya mjumbe huyo wa Hizbullah katika Bunge la Lebanon yanatolewa katika hali ambayo kumekuwepo na propaganda kwamba harakati hizo mbili zimekuwa na mivutano mikubwa hususan juu ya kadhia ya Syria, suala ambalo linatajwa kuwa halina ukweli wowote.