Wasiwasi wa kutokea ghasia watanda Sudan, bei ya nishati imeongezwa
Kuongezwa kwa bei ya nishati nchini Sudan kumezidisha wasiwasi wa kutokea ghasia na maandamano ya wananchi dhidi ya serikali ya nchi hiyo.
Ripoti zinasema kuwa serikali ya Khartoum Ijumaa ya jana ililiamuru jeshi la polisi na askari usalama kuwa katika hali ya tahadhari kwa kuchelea maandamano na malalamiko ya wananchi baada ya kupandishwa juu bei ya nishati.
Mkuu wa Kituo cha Masuala ya Idara na Mipango cha Polisi ya Sudan, Babakr Mustafa ametangaza kuwa, askari usalama wa nchi hiyo wamewekwa katika hali ya tahadhari kwa ajili ya kuzuia malalamiko ya wananchi.
Ripoti zinasema magari ya polisi yanaolena kwa wingi yakifanya doria katika mita ya mji mkuu wa Sudan, Khartoum na idadi ya polisi imeongezeka.
Wataalamu wa masuala ya uchumi wanasema kupandishwa kwa bei ya nishati kutazidisha bei ya bidhaa muhimu kwa zaidi ya asilimia mia moja, suala ambalo wanasisitiza kuwa, matokeo yake ni kuongezeka hasira na upinzani wa wananchi dhidi ya serikali ya Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo.
Wachambuzi wa mambo pia wanatahadharisha kuwa, hatua hiyo yumkini ikakwamisha mazungumzo ya kitaifa nchini Sudan.