Rais wa Guinea-Bissau amfuta kazi Waziri MKuu na kuvunja tena serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19504-rais_wa_guinea_bissau_amfuta_kazi_waziri_mkuu_na_kuvunja_tena_serikali
Kwa mara nyingine tena Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amemfuta kazi Baciro Dja, Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuivunja serikali, ikiwa ni katika juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 15, 2016 04:38 UTC
  • Rais wa Guinea-Bissau amfuta kazi Waziri MKuu na kuvunja tena serikali

Kwa mara nyingine tena Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau amemfuta kazi Baciro Dja, Waziri Mkuu wa nchi hiyo na kutangaza kuivunja serikali, ikiwa ni katika juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa uliopo.

Akihutubia waandishi wa habari hapo jana katika mji mkuu Bissau, Rais Vaz amesema ameivunja serikali ya Baciro Dja, kufuatia makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili hasimu za kisiasa huko Conakry, mji mkuu wa nchi jirani ya Guinea Conakry mwezi uliopita.

Rais José Mário Vaz wa Guinea-Bissau

Amesema mwafaka huo unaofahamika kama Makubaliano ya Conakry ulipendekeza kupigwa kalamu nyekundu Waziri Mkuu na kuvunjwa serikali, sambamba na kuteua serikali nyingine. Hata hivyo makubaliano hayo hayajaainisha tarehe ya kuchagua serikali mpya ingawa duru za karibu na rais huyo zinasema kuwa, uteuzi huo utafanyika wakati wowote kuanzia sasa.

Itakumbukwa kuwa, mwezi Mei mwaka huu, rais huyo alimpiga kalamu Carlos Correia, Waziri Mkuu wa wakati huo na kutangaza kuivunja serikali.

Baciro Dja, Waziri Mkuu aliyepigwa kalamu Guinea-Bissau

Baciro Dja kama wenzake watatu waliomtangulia, alitazamiwa na utawala wa Rais Vaz kuupatia ufumbuzi mzozo wa kisiasa unaotokota nchini humo unaodaiwa kuripuka kuanzia ndani ya chama tawala cha PAIGC.

Mgogoro wa kisiasa nchini Guinea-Bissau ulishadidi Agosti mwaka jana 2015, baada ya Rais Vaz kumfuta kazi Domingos Simoes Pereira, kiongozi wa chama tawala.