Kenya yaakhirisha tarehe ya kufunga kambi ya Dadaab
Kenya imerefusha muda wa kuwarejesha makwao wakimbizi wa Somalia walioko katika kambi ya Dadaab iliyoko kaskazini mashariki mwa nchi, ambayo ilitazamiwa kufungwa kikamilifu kufikia mwishoni mwa mwezi huu.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Joseph Nkaissery amesema shughuli ya kuwarejesha nchini kwao wakimbizi hao sasa itaendelea kwa muda wa miezi sita zaidi.
Licha ya kuwa hatua hiyo ya serikali ya Nairobi inaonekana kuchukuliwa kutokana na mashinikizo ya jamii ya kimataifa, lakini Nkaissery amewaambia waandishi wa habari mjini Nairobi kuwa, uamuzi huo ni wa kibinadamu ili kuwapa muda zaidi wakimbizi hao wa Kisomali kutafuta makazi mbadala na kubainisha kuwa, serikali haitawazuia wanaotaka kurejea nchini kwao kwa hiari.
Julai mwaka huu, operesheni ya kuwarejesha makwao wakimbizi hao ilianza licha ya kuwepo juhudi za kimataifa za kutaka kuzuia zoezi hilo. Mwezi mmoja kabla ya hapo Kenya ilitangaza kuwa itafunga kambi hiyo na kubainisha kuwa, kwa karibu miaka 25 sasa nchi hiyo imekuwa ikiwahudumia wakimbizi wapatao laki sita kutoka nchi jirani na hasa Somalia ambapo imegharamika pakubwa kiuchumi, kiusalama na kimazingira katika kuwadhaminia mahitaji yao ya kimsingi, jambo ambalo imesema haina tena uwezo wa kuendelea kulifanya.
Mbali na raia wa Somalia, wakimbizi wengine kutoka nchi jirani wakiwemo raia wa Uganda, Eritrea, Sudan Kusini na Ethiopia pia wanaishi kwenye kambi hiyo kubwa zaidi duniani.