Rais el-Sisi atoa msamaha kwa wafungwa vijana 82 nchini Misri
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19720-rais_el_sisi_atoa_msamaha_kwa_wafungwa_vijana_82_nchini_misri
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametoa msamaha kwa wafungwa vijana 82 waliokuwa wakitumikia vifungo vyao jela.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 18, 2016 11:22 UTC
  • Rais el-Sisi atoa msamaha kwa wafungwa vijana 82 nchini Misri

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametoa msamaha kwa wafungwa vijana 82 waliokuwa wakitumikia vifungo vyao jela.

Maafisa wa idara ya wafungwa nchini Misri wametangaza leo kuwa, wafungwa hao walioapata msamaha wa rais, wanatoka katika jela tofauti za nchi hiyo. Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na ikulu ya Rais el-Sisi, wengi wa walionufaika na msamaha huo, ni wanafunzi wa vyuo vikuu. Ofisi ya habari ya rais huyo anayetuhumiwa kwa ukandamizaji na ukanyagaji wa haki za binaadamu nchini Misri, imeongeza kuwa, msamaha huo umetolewa kwa mujibu wa kifungu 155 cha katiba, ambacho kinampa idhini rais kutoa msamaha kwa wafungwa.

Wafungwa nchini Misri

Itakumbukwa kuwa, baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Rais Muhammad Mursi mwaka 2013, yaliyoongozwa na Jenerali wa kijeshi Abdel Fattah el-Sisi, Misri ilikumbwa na wimbi la maandamano ya wananchi waliopinga mapinduzi hayo. Katika harakati hizo, maelfu ya watu wakiwemo wanafunzi walitiwa nguvuni na kuhukumiwa vifungo jela, huku mamia ya wengine wakiuawa na kujeruhiwa. Kufuatia hali hiyo, asasi mbalimbali za kutetea haki za binaadamu zilimtuhumu rais huyo kwa ukandamizaji dhidi ya binaadamu nchini Misri.