Rais wa Zambia ajipunguzia mshahara kwa asilimia 50
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i19765-rais_wa_zambia_ajipunguzia_mshahara_kwa_asilimia_50
Rais Edgar Lungu wa Zambia ametangaza kupunguza mshahara wake kwa asilimia 50, ikiwa ni katika hatua ya serikali yake ya kujaribu kubana matumizi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 19, 2016 04:30 UTC
  • Rais wa Zambia ajipunguzia mshahara kwa asilimia 50

Rais Edgar Lungu wa Zambia ametangaza kupunguza mshahara wake kwa asilimia 50, ikiwa ni katika hatua ya serikali yake ya kujaribu kubana matumizi.

Makamu wa Rais wa Zambia, Inonge Wina ameliambia bunge la nchi hiyo kuwa, Rais Lungu ataanza kupokea nusu ya mshahara ambao amekuwa akiupokea wa dola 3,645 za Marekani.

Makamu wa Rais wa Zambia amewaomba wabunge na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini kukubali kupunguziwa mishahara yao kwa ajili ya kuunusuru uchumi wa nchi hiyo unaoyumba. Amesema kuwa asilimia 50 ya mshahara wa Rais Edgar Lungu itaenda katika maswala ya misaada na 'sadaka'.

Wafuasi wa Rais Lungu katika uchaguzi uliopita

Zambia ambayo ina takriban watu milioni 14.5, ilisoma bajeti ya mwisho ya dola bilioni 6.6 za Marekani huku Waziri wa Fedha Felix Mutati akiapa kuchukua hatua kadhaa za kukabili ukosefu wa ajira, mgogoro wa umeme na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama chakula, katika nchi hiyo inayotegemea zaidi madini ya shaba nyekundu (copper). 

Ni vyema kukumbusha kuwa, uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Agosti mwaka huu huko Zambia ulikuwa wenye ushindani mkali kati ya rais wa sasa wa nchi hiyo Edgar Lungu na mgombea wa upinzani Hakainde Hichilema ambaye alidai kuibiwa kura.

Rais Edgar Lungu wa Zambia

Itafahamika kuwa, Zambia ni moja ya nchi za Kiafrika ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimekumbwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kiusalama.